May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DKT. Tulia aiagiza kamati ya ipu kushughulikia mgogoro wa Israel na Palestina

Na Mwandishi Wetu 

RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameielekeza Kamati inayoshughulikia Masuala ya Mashariki ya Kati ya Umoja huo kutembelea eneo hilo mapema katika juhudi za kutafuta suluhusho linaloweza kuhakikisha amani na usalama vinapatikana kufuatia mgogoro unaoendelea baina ya Israel na Palestina. 

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 30 Novemba, 2023 Jijini Tel Aviv nchini Israel mara baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili iliyompa fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Viongozi mbalimbali wa Israel na Mamlaka ya Palestina.

“Nimekuja kutembelea maeneo ya Palestina na Israel ambao wote hawa mabunge yao ni Wanachama wa IPU lakini muhimu zaidi kuwafahamisha kuwa tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na Kamati yetu inayoshughulikia Masuala ya Mashariki ya Kati itakuwa hapa siku zijazo kutafuta uhalisia wa mgogoro huu na kuleta taarifa ambayo tutapata nafasi ya kuijadili ili tuone huko mbele tunakokwenda tunawezaje kuwa na amani na usalama kwa watu wote.” Dkt. Tulia

Amefafanua kuwa, moja ya msingi wa IPU ni kuhakikisha uhai wa kila binadamu unalindwa na Umoja huo utafanya kila linalowezekana ili dunia iwe sehemu salama na ya amani kwa binadamu wote bila kujali rangi, itikadi, imani na maeneo wanayotoka. 

Aidha amesisitiza kuwa, Mpango mkakati wa Umoja huo ni kuutumia Mwaka 2024 pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina suala la Amani na Usalama kama ajenda muhimu kwenye Mikutano yake Mikuu ya mwezi Machi na Oktoba mwakani. 

Katika ziara hiyo Dkt. Tulia na ujumbe wake amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Mamlaka ya Palestina Jijini Ramallah akiwemo Waziri Mkuu wa Mamlaka hiyo Mhe. Muhammad Shtayyeh pamoja na Spika wa Baraza la Mamlaka ya Palestina Mhe. Rawhi Fattouh.

Vilevile Dkt. Tulia alipata fursa ya kutembelea Kijiji cha Kfar Aza Kibbutz kati ya vijiji vilivyoshambuliwa na wanamgambo wa Hamas Oktoba 7, 2023 na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Israel (Knesset) Mhe. Amir Ohana, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Vijiji Mhe. Avi Dicter na Wabunge Wawakilishi wa Knesset kwenye IPU walioongozwa na Mhe. Danny Daddon.