May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DKT. Yonazi-Viongozi wa Dini tumieni majukwaa yenu kuhamasisha waumini na jamii katika mwitikio wa UKIMWI

Na Mwandishi wetu 

VIONGOZI wa dini nchini wamehimizwa kuwaelimisha na  kuwajenga vijana katika maadili mema, kuwaepusha na maambukizi ya VVU na kudhihirisha jitihada za pamoja kati ya Taasisi za dini na Serikali katika kulinda na kuhamasisha vijana kutambua hali zao za maambukizi ya VVU na kupata elimu ya  Afya ya Uzazi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri  Mkuu  Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi katika    ufunguzi wa Mdahalo kati ya Vijana na Viongozi wa dini uliofanyika Novemba  29, 2023 mkoani Morogoro ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea kuelekea kilele cha maadhimisho ya  siku ya UKIMWI itakayofanyika Desemba Mosi mwaka huu.

Dkt. Yonazi amesema  kufanyika kwa mdahalo huo iwe chachu ya  kuhamasisha na kutetea mitazamo chanya katika kupinga unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI na kuwa na mkakati maalumu kuhakikisha kuwa Nyenzo na Miongozo  iliyopo inatumika ipasavyo.

“Takwimu zinaonesha kuwa moja ya makundi yaliyo nyuma katika kufikia malengo yaliyowekwa  ya Sifuri tatu ni kundi la VIJANA. Hii ni kwa kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kwenye afua za VVU na UKIMWI, vijana wengi wenye umri wa miaka 15-24 hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa,”Amesema Dkt. Yonazi.

Pia ameongeza kwamba Katika kufikia lengo la sifuri ya maambukizo mapya kama nchi, maambukizi mapya yameendelea kushuka mwaka hadi mwaka, akisema hadi sasa   takwimu zinaonesha kuwa takribani watu 54,000 waliambukizwa VVU mwaka 2021 nchini ambapo ni  sawa na takribani watu 4,500 kwa mwezi au watu 150 kwa siku.

“Vijana wenye umri wa miaka 15-24 ndio kundi ambalo linaonesha kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizo mapya, kwani katika watu wote wanaopata maambukizi mapya ya VVU kila mwaka, takribani asilimia 35 ni vijana wenye umri wa miaka 15-24 (yaani katika kila watu 10 wanaopata maambukizo mapya ya VVU watatu ni vijana wa umri huu na takribani asilimia 74 ni wasichana,”Amefafanua.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amebainisha baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa vijana kuwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa Dini kuwazuia watu wanaoishi na VVU kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi kutokana na imani kwamba maombi pekee au uponyaji wa kimiujiza pekee ndivyo vinavyokubalika.

“Baadhi ya watu wanaoishi na VVU huacha matibabu kutokana na mafundisho na matamko ya baadhi ya viongozi wa Dini, Baadhi ya viongozi wa Dini kutotoa tahadhari ya kutosha kuhusu mahitaji maalum ya vijana wanaoishi na VVU na changamoto wanazokumbana nazo zinazohusiana na matibabu,” Ameeleza.

Vivile Dkt. Yonazi  ametoa rai kwa viongozi wa Dini akiwataka kutumia majukwaa yao kutoa elimu ili kusaidia kuhamasiaha waumini na jamii ambao ni watoto, vijana na watu wazima katika mwitikio wa UKIMWI hatua itakayosaidia  kuongeza uelewa katika jamii kuhusu ufuasi mzuri wa dawa na matibabu, kuhamasisha upimaji na kwa baadhi ya wazazi ambao hawawaweki wazi watoto wao ambao wapo kwenye matumizi ya dawa, na kusaidia katika mapambano dhidi ya unyanyapaa na ubauguzi na ukatili wa kijinsia.

“Hii itaiwezesha nchi yetu kufikia malengo ya TISINI NA TANO (95%) TATU ifikapo 2025 katika mapambano dhidi ya VVU na  Asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizo; asilimia 95 ya waliopimwa VVU na kugundulika kuwa wana maambukizo watumie dawa za kufubaza VVU (ARV) na asilimia 95 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU),”Amesema Dkt. Yonazi.

Ikumbukwe maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani hufanyika kila mwaka ambapo mwaka huu Kitaifa yatafanyika mkoani Morogoro Desemba Mosi mwaka 2023 chini ya kauli mbiu isemayo “Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI”