Na Omary Mtamike,TimesMajira Online,Kilimanjaro
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah imesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi na matumizi yake kimeongezeka ukilinganisha na kile kilichokuwepo mwaka 2020.
Dkt. Tamatamah ameyasema hayo jana wakati akisoma taarifa ya Wizara hiyo kwenye sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambazo kitaifa zimefanyika mkoani Kilimanjaro kwenye Uwanja wa shule ya Msingi Nelson Mandela uliopo eneo la Pasua Manispaa ya Moshi.
“Kiwango cha uzalishaji wa samaki kupitia maji ya asili kwa mwaka 2021 kimefikia takribani tani 372,000 huku uzalishaji wa mazao hayo kwa tasnia ya ufugaji wag samaki ukifikia takribani tani 20,355 na wastani wa kiwango cha ulaji wa samaki hao kimeongezeka kutoka kilo 8.2 hadi kilo 8.5 kwa mtu kwa mwaka ” amesema Dkt. Tamatamah.
Akizungumzia kwa upande wa sekta ya Mifugo, Dkt. Tamatamah amesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa nyama kimeongezeka hadi tani 738,166 ukilinganisha na tani 701679 zilizozalishwa mwaka uliopita na kiwango cha uzalishaji wa maziwa kimefikia lita bilioni 3.4 ikilinganishwa na lita bilioni 3.1 zilizozalishwa mwaka uliopita.
Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa kuongezeka kwa kiwango hicho cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kumetokana na dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na uhaba wa chakula na lishe bora hapa nchini.
“Aidha maadhimisho haya ya Siku ya Chakula nchini huwa ni moja ya chachu za kuongeza uzalishaji wa mazao haya ya mifugo na uvuvi kwa sababu hutukumbusha kuwatendea haki wananchi kwa kuhakikisha chakula cha kutosha na chenye ubora kinapatikana na kinalindwa ili kisiharibike kabla au baada ya kuvunwa ili kimfikie mlaji kikiwa salama” Ameongeza Dkt. Tamatamah.
Hata hivyo Dkt. Tamatamah amewasihi wananchi kuendelea kutumia vyakula vinavyotokana na mazao ya mifugo na Uvuvi kwa wingi ili kufikia viwango vilivyowekwa na Shirika la Umoja wa mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ambalo husisitiza kila mtu kula wastani wa kilo 20.3 za samaki, kilo 50 za nyama na lita 200 za maziwa kwa mwaka.
Maadhimisho ya Siku ya chakula Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kumkumbusha mwananchi kuzingatia lishe bora wakati wote ili kuondokana na changamoto ya tatizo la udumavu na kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora wakati wote.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi