November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Sengati amrithi Mwanri Tabora, Gondwe ahamishiwa Temeke

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ikulu, Chamwino

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 03 Julai, 2020 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mkoa 2 kama ifuatavyo;

Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dkt. Philemon Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Kabla ya uteuzi huo, Dkt. Sengati alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza na anachukua nafasi Bw. Aggrey Mwanri ambaye amestaafu.

Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Thobias Andengenye (aliyewahi kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji) kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Bw. Andengenye anachukua nafasi ya Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga ambaye amestaafu.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 9 kama ifuatavyo;

Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Ismail Twahir Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.

Kabla ya uteuzi huo, SACP Mlawa alikuwa Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Morogoro na anachukua nafasi ya Bw. James Mugendi Ihunyo ambaye amestaafu.

Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bi. Jamila Yusuf kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi.

Kabla ya uteuzi huo, Bi. Jamila Yusuf alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma na anachukua nafasi ya Bi. Lilian Charles Matinga ambaye amestaafu.

Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua Mhandisi Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.

Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Ntemo alikuwa Mhandisi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na anachukua nafasi ya Asumpter Nshunju Mshama ambaye amestaafu.

Nne, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Salum A. Kali kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza.

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Kali alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza na anachukua nafasi ya Dkt. Philemon Sengati ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Tano, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Wilson Samwel Shimo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Mkoani Geita.

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Shimo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida.

Sita, Mhe. Rais Magufuli amemteua Kanali Mathias Kahabi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera.

Kanali Kahabi anachukua nafasi ya Saada Malunde ambaye amestaafu.

Saba, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Abbas Kayanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Kayanda alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu na anachukua nafasi ya Bi. Theresia Jonathan Mahongo ambaye amestaafu.

Nane, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Lazaro Jacob Twange kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara.

Bwana Twange anachukua nafasi ya Bi. Elizabeth Simon Kitundu ambaye amestaafu.

Tisa, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Toba Alnason Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni

Kabla ya uteuzi huo, Bw. Nguvila alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido Mkoani Arusha na anachukua nafasi ya Bw. Godwin Gondwe ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam.

Bw. Godwin Gondwe anachukua nafasi ya Bw. Felix Jackson Lyaniva ambaye amestaafu.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza leo tarehe 03 Julai, 2020 na wateule wote wanatakiwa kuwepo Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 06 Julai, 2020 saa 4:00 asubuhi.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chamwino

03 Julai, 2020.