January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Ndumbaro: Sheria nzuri za habari zitawezesha kukuza haki ya kupata habari

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema, sheria nzuri za habari zitawezesha kukuza haki ya kupata habari, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kutoa maoni itakayozalisha maendeleo ya haraka kwa nchi.

Kauli hiyo ameitoa jijini Arusha hivi karibuni alipokutana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI).

Akizungumza na wajumbe hao Waziri Ndumbaro amesema Rais Samia Suluhu Hassan tayari ameonesha dhamira ya dhati ya kutetea sauti ya vyombo vya habari, yupo tayari kutoa haki za vyombo vya habari na waandishi wa habari pia hivyo kwa sasa ni wakati mzuri wa kulisukuma suala la mabadiliko ya sheria ya habari.

Pia amesema yeye na wabunge wenzake watashiriki vyema katika mchakato wa kulipatia taifa sheria za habari zilizo bora na zitazodumu kwa muda mrefu.

Mbali na hayo Ndumbaro amewataka TEF kufanya mazungumzo ya ukaribu na waziri Nape Nnauye ili aweze kulisukuma kwa haraka suala hili la sheria za habari.

“Waziri Nape akiwaelewa, anayo nafasi kubwa ya kulisukuma suala hili na mkabadili sheria zinazolalamikiwa ndani ya muda mfupi. TEF na wadau wengine hakikisheni mnazungumza kwa karibu na Waziri Nape,” amesema.