May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

OMH yajivunia kuvuka lengo ukusanyaji mapato yasiyo ya kodi kwa asilimia 109.5

OFISI ya Msajili wa Hazina imevuka lengo la kukusanya sh.bilioni 779.09 sawa na asilimia 33.5 na kukusanya sh.bilini 852.98 sawa na asilimia 109.5 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2022 ambapo ni zaidi ya kiasi kilichokusanywa Juni 30 mwaka 2021 ambacho kilikua ni sh.bilioni 638.87.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Umma Ofisi ya Msajili wa hazina,Lightness Mauki wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Msajili wa Hazina,Mgonya Benedicto kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali na mwelekeo wa utekelezaji katika kipindi cha mwaka 2022/23.

Ambapo amesema kua huo ni ufanisi mkubwa, unaotia moyo na ambao haujawahi kufikiwa na Ufanisi huo umechangiwa na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya uwekezaji wa mitaji ya Umma, hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali katika kukuza mapato na kudhibiti matumizi pamoja na kuongezeka kwa shughuli za ufuatiliaji katika Taasisi, Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa chache.

“Pamoja na jitihada zinazoendelea za kuimarisha usimamizi wa Mashirika, Wakala za Serikali na Taasisi za Umma bado kumekuwa na dhamira  ya kuzidi kuongeza tija zinazotokana na Mashirika hayo ili Serikali iweze kupata rudisho la uwekezaji wake kwa faida ya wananchi na Taifa kwa ujumla,”amesema Mauki.

Mauki amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea na juhudi za kusimamia utendaji wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano na wabia wenza na kusimamia kwa karibu matumizi yasiyo ya lazima ambapo ongezeko la gawio kwa wanahisa limeonekana.

Amesema kuwa mafanikio ya jitihada hizo yamejidhihirisha katika utendaji wa benki ya NBC ambayo imeongeza faida kabla ya kodi kutoka Shilingi bilioni 7 mwaka 2020 hadi Shilingi bilioni 60 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 757. 

“Ukuaji huu wa faida umewezesha benki hii kutoa gawio kwa serikali Shilingi Billioni 4.5 kiasi ambacho hakijawai kufikiwa,”amesema. 

Aidha amesema mapato kutoka Kampuni ya Airtel yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 34.66 mwaka 2020/21 hadi kiasi cha Shilingi bilioni 104.22 mwaka 2021/22. 

“Mapato haya yanajumuisha ulipaji wa gawio na utekelezaji wa makubaliano maalumu ya wanahisa pia kwa  Benki ya NMB imetoa kwa Serikali gawio la kiasi cha shilingi Billioni 30.7 kutoka Billioni 21.7 ya mwaka 2020/21 na haya ni baadhi ya mafanikio makubwa yaliyotokana na uimarishwaji wa mahusiano ya kiutendaji baina ya wanahisa,”amesema.

Akizungumzia mafanikio ya OMH,Mauki amesema kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya kiwanda baada ya kufanya uchambuzi wa kina iliwasilisha mapendekezo ya kupanua kiwanda kwa wanahisa, ambapo Serikali kupitia Msajili wa Hazina pamoja na wanahisa wenza (Illovo Group) baada ya majadiliano waliafiki kutekeleza mradi mkubwa wa upanuzi wa kiwanda kwa gharama ya kiasi cha Shilingi bilioni 571.6 (Dola za marekani milioni 238.5). 

Ameeleza kuwa Uwekezaji huo unatarajiwa kuzalisha sukari tani 144,000 ambazo zitaongeza uwezo wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kuzalisha sukari hadi kufikia tani 271,000 kutoka tani 127,000 za sasa. 

“Utekelezaji wa mradi huu tayari umeanza na unatarajiwa kuwa na mafanikio makubwa kwa njia ya kuongeza ajira, kuinua kipato kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo, gawio kwa wanahisa na kichocheo cha uchumi kwa ujumla,”amesema.

Mauki ameeleza kuwa Serikali ni mbia katika Kiwanda cha Sukari Kilombero ambapo ina umiliki wa asilimia 25 kupitia Msajili wa Hazina.