May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Ndumbaro aagiza timu za Ligi kuu kuwakatia Bima za Afya wachezaji

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amelielekeza Baraza la Michezo la Taifa “BMT” kuhakikisha kuwa ifikapo Januari, 2024 kila klabu ya ligi kuu ya NBC iwe na Bima ya afya kwa wachezaji wake na iingizwe kwenye Kanuni ili kuwalinda wachezaji.

Mhe. Dkt. Ndumbaro amesema hayo Desemba 6, 2023 jijini Dar Es Salaam kwenye uzinduzi wa Taarifa ya Maendeleo ya Soko la Bima kwa Mwaka 2022.

“Kuanzia Januari mosi timu zote za Ligi Kuu zikate bima kwa wachezaji wote na hilo nikuagize Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msitha hilo liingizwe kwenye kanuni tuwalinde wachezaji waweze kufanya vizuri,”amesema.

Aidha, Mhe. Ndumbaro amesema sekta ya michezo ina watu wengi sana hivyo ni muhimu kwa kampuni za bima kuangalia upande huo na kuwatumia kama sehemu ya kujitangaza.

Awali, Kamishna wa Bima wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima “TIRA” Dkt. Baghayo Saqware amesema soko la Bima limekua kufikia trilioni 1.158 mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.7

Ameshukuru Makampuni ya bima kwa kazi nzuri waliofanya ya kuongeza mapato na kulinda usalama wa mali na afya ya jamii.

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizindua Taarifa ya Maendeleo ya Soko la Bima kwa Mwaka 2022 hapo Jana Jijini Dar es Salaam