Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameendelea kusisitiza juu ya dhamira njema ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga sekta binafsi imara ambayo itachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu jijini Dar es Salaam chini ya Rais Samia, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza hilo, Waziri Nchemba amesema ndani ya siku 90 tangu kuapishwa kwake kushika huo, Rais amefanikiwa kujenga matumaini makubwa kwa sekta binafsi ambayo ndio injini ya maendeleo ya nchi.
“Kwa muda mfupi tangu kuapishwa kwake ameonesha wazi dhamira yake ya kujenga sekta binafsi yenye nguvu na imara na itakayoweza kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi,” amesema Waziri Nchemba na kuyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na marekebisho ya mifumo ya kikodi ambayo yamefanyika kwenye Bunge la Bajeti.
Waziri Nchemba amesema marekebisho hayo yamelenga kukuza uchumi wa nchi, kuongeza mapato pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi.
“Maboresho ambayo yamefanyika yatasaidia kuongeza makusanyo ya kodi na kukua kwa biashara kwa kuwa fedha itakuwepo mikononi mwa watu jambo ambalo litachochea zaidi uzalishaji na hivyo kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania,’’ alieleza.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza, Dkt. Godwill Wanga, amesema mkutano huo umefanyika kwa mafanikio makubwa kwa kupata masuluhisho ambayo yataleta manufaa kwa pande zote mbili ambazo ni sekta ya umma na sekta binafsi.
“Mkutano umeendeshwa vizuri na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza na ametoa maagizo kadhaa katika maeneo ambayo yalionekana bado yana changamoto pamoja na kuja na masuluhisho ambayo yatakuwa muhimu kwa ufanyaji biashara na uwekezaji,” alisema Dkt. Wanga.
Amesema miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na kuhakikisha kodi zisizo na tija zinaondolewa ili kutanua wigo wa kodi, kuendeleza viwanda vya bidhaa za misitu, kufanyika kwa maboresho ya mabaraza ya mikoa na wilaya pamoja na kuzifanya sekta binafsi ziweze kukopo kwenye mabenki ili kuimarisha mkakati wa ubia kati ya sekta za umma na binafsi (PPP).
Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Kilimo ya TNBC, Jacqueline Maleko, amesema usikivu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika masuala ya ukuzaji wa biashara na uwekezaji yataipasha nchi kimaendeleo.
“Kama sekta binafsi, tumehamasika na usikivu wa Rais Samia ambaye yupo tayari kuijenga sekta binafsi kwa manufaa ya nchi. Wakati umefika kushirikiana na sekta ya umma kupitia vyombo vyetu kama TNBC, Taasisi ya sekta Binafsi (TPSF) na vingine vingi ambavyo tunaweza kupeleka changamoto zetu serikalini,” alisema Jacqueline.
Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) lilianzishwa na Serikali mwaka 2001 kama jukwaa rasmi la majadiliano kati sekta binafsi na umma ili kuondoa hali ya kutoaminiana na tayari mafanikio mengi yamepatikana ikiwemo mabadiliko ya sera, kanuni na sheria.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati