Na Mwandishi Wetu, Timesmajira online, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itawachukulia hatua za kisheria watumishi kutoka taasisi na mashirika ya umma walioshindwa kutoa majibu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti ya mwaka wa fedha 2022- 2023 iliyowasilishwa na kusomwa Ikulu, Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza kwenye viwanja vya Ikulu, Zanzibar baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Kuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar, (CAG).
“Ninataka kupata majibu kwa wote waliotajwa kwenye ripoti ya CAG ambao hawakutoa majibu, watoe ambao watashindwa kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa,”amesisitiza Rais Dkt. Mwinyi.
Amesema, ripoti imeonesha mafanikio, changamoto na mapungufu ambayo ofisi ya CAG iliyabainisha wakati wa uwasilishwaji wake na kueleza kwamba serikali itachukua hatua mbalimbali zikiwemo za kiutawala na kijinai kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa.
“Kwa wale wote watakaothibitika kufanya ubadhirifu, wizi au uzembe ulioisababishia serikali kupata hasara, utaratibu wa kuchukua hatua uko wazi,”amebainisha Dkt. Mwinyi.
Pia amesema, kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kuchukuliwa hatua za kiutawala na baadhi ya kuchukuliwa hatua za sheria za makosa ya jinai.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba ataikabidhi ripori hiyo kwa mamlaka zinazohusika kwa hatua zaidi, ikiwemo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi, Zanzibar (ZAECA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili nao waipitie kwa kina mapungufu yote hasa yaliyoashiria wizi kwa ajili ya hatua zaidi kwa mujibu wa sheria.
Dkt.Mwinyi amesema, ripoti za CAG ni kipimo tosha cha utendaji kwa wale wote waliopewa majukumu na Serikali kwa kufanikiwa ama kushindwa kuyasimamia katika kuitumikia Serikali.
“Utaratibu huu tuliouazisha wakuwasilisha ripoti za CAG hadharani utakuwa wakudumu, nafahamu kuwa haukuzoeleka na unawapa mashaka baadhi ya watu, nataka niwahakikishie kwa wale wenye mashaka, hili litakua zoezi la kila mwaka, na ni moja wapo ya kigezo cha uwazi na utawala bora katika uendeshaji wa Serikali yetu,”amebainisha Dkt.Mwinyi.
Hata hivyo, aliwataka watendaji na watumishi wa taasisi na mashirika ya serikali kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa ofisi ya CAG Zanzibar panapokua na wajibu wa kufanya hiyo na kutofanya hivyo ni kosa kisheria na Serikali haitosita kutimiza wajibu wake.
Akizungumzia mapungufu yaliyojitokeza kwenye ripoti hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa baadhi ya mapungufu hayo ni ya kiutaratibu, mengi yalisababishwa na wizi na mengine uzembe kwa baadhi ya watu.
Hivyo ameeleza kuwa kazi ya CAG ni kutoa taarifa na mapendekezo kwa Serikali na jukumu la kufanyiakazi ripoti hiyo ni la Serikali.
Akiwasilisha ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dkt.Othman Abass Ali, ameishauri Serikali kuunganisha pamoja mifumo yote ya fedha ya Serikali, kwa miamala ya fedha zikiwemo fedha zilizoko Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kupitia mifumo ya Wizara ya Fedha kwa lengo la kuiwezesha mifumo hiyo, kufanya usuluhishi wa upatikanaji wa taarifa za ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa wakati sahihi.
Sambamba na kuziunganisha pamoja sekta zote za Serikali zinazofanyakazi zinazofanana katika mfumo mmoja zikiwemo, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA), Kampuni ya Usafirishaji bandarini na nyenginezo ili kupata idadi kamili ya wageni na abiria wanaoondoka Zanzibar kwa lengo la kuwepo kigezo sahihi cha ukokotoaji wa ukusanywaji wa mapato yanayotakiwa kupatikana kutoka kwenye vyanzo hivyo.
Pia ameishauri serikali kuongeza udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi, ikiwemo kufanya uteketezaji pamoja na kuvipitia vituo vyote vya afya kwa hospitali zote za Wilaya, Mikoa hadi Rufaa kwa dawa zilizomo hospitalini.
Pamoja na kufanya vipimo vya kimaabara ili kugundua dawa na vifaa visivyo salama kwa matumizi wa binaadamu kwa kuzichukulia hatua za haraka na kuziondosha kwa kuziteketeza kwa wakati.
Akizungumzia suala la kulipa fidia kwa wananchi wanaotoa maeneo yao kwaajili ya kupisha miradi ya serikali ya maendeleo, CAG ameishauri serikali kuona umuhimu wa kuwalipa kwa wakati ili kuepusha malalamiko, kucheleweshewa kulipwa kwa wakati kunapunguza thamani ya fidia kutokana na kupungua kwa thamani ya fedha.
Jumla ya ripoti saba ikiwemo ya Serikali Kuu (Wizara na taasisi zote),mashirika na taasisi zinazojitegemea, ripoti ya idara maalum na taasisi zake, ripoti ya mifumo yote ya tehema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ripoti ya Mashirika ya Umma, na ripoti ya Ufanisi ya miradi ya Maendeleo iliyofadhiliwa na fedha za Uviko-19 ziliwasilishwa.
Kifungu cha 112 (5) kinamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, awasilishe taarifa yote aliyoikagua na aikabidhi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa hatua nyengine.
Mei 11 mwaka huu alifanya hivyo na baadae Rais Dk. Mwinyi alimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman ambae nae alikabidhi kwa Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa takwa la kikatiba kwaajili ya kujadiliwa.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa