May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mutahabwa:Vitisho kwa wanafunzi vinaua elimu ya Tanzania

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Kamishna wa elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema vitisho mashuleni katika ngazi ya awali mpaka vyuo vikuu ikiwemo viboko vya kila wakati vinaua elimu ya Tanzania.

Hayo aliyasema jana wakati wa kikao kilichowakutanisha walimu kutoka vyuo 35 vya ualimu nchini kutathmini mradi wa kuendeleza elimu ya walimu (TESP na UTC) uliofadhiliwa na serikali ya Canada ambao ulianza mwaka 2017 na unatarajiwa kudumu kwa miaka saba unaolenga kuleta maboresho katika mafunzo ya walimu Tanzania na kujenga miundombinu katika vyuo vya ualimu.

“Kitendo cha kutumia kiboko wakati wote ukizani ya kwamba utawafanya wanafunzi wapende kusoma na kufaulu si mtazamo sahihi”

“Kwa uzoefu wangu kama mwalimu mimi nimekua nikiwafundisha wanafunzi darasani kwa kuwakumbatia wanafunzi wote kwa upendo na kujua ya kwamba wanafunzi hawalingai uwezo kila mwanafunzi amejaaliwa neema yake kwa hiyo nawachukulia wote kama walivyo na kutafuta mbinu mbalimbali za kumsaidia kila mmoja njaa na kiu yangu ni kwamba kama wanafunzi walianza wakiwa 200 basi wote wamalize waende mbele” Aliongeza Dkt.Mtahabwa.

Dkt. Mtahabwa alisema Mradi wa TESP na UTC utasaidia sana katika kuwabadilisha walimu kuona kwamba ualimu ni kazi ya thamani na inapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa.

Aidha Dkt. Mtahabwa alisema Mradi huo umewezesha kuunganisha vyuo vya ualimu kwenye mkongo wa Taifa lakini pia umeboresha mafunzo ya walimu kwa vitendo.

“Mwalimu bora ana kiu ya kujifunza kila leo pamoja na mafunzo kazini, mradi huu umewezesha ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo vitabu, umewezesha kuboresha maktaba zetu , maabara na Labaratory za ICT”

Dkt. Mtahabwa alisema baada ya siku kadhaa wataangalia nini kimefanyika ndani ya Mradi huo na kuweka mikakati ya namna ya kuuendeleza miradi hiyo ili yale mazuri yote yasikwamie Tanzania bali yaendelee na nchini zingine lakini pia hata baada ya Mradi kuisha.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa kuendeleza elimu ya walimu (TESP), Cosmas Mahenge alisema mradi huo unaendeshwa na wizara ya elimu ambapo pesa zinazotolewa na serikali ya Tanzania zinasaidia gharama za chakula kwa wanavyuo katika vyuo vyote vya a ualimu 35 lakini pia inachangia kwa upande wa fedha za mafunzo kwa vitendo na kwa Canada wametoa pesa ili zitumike katika shughuli mbalimbali.

“Kazi kubwa iliyofanyika na Mradi ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wakufunzi takribani 1300 wa vyuo vya ualimu na wote wameweza kupatiwa mafunzo ikiwemo mafunzo ya TEHAMA, usawa wa kijinsia, mafunzo ya masomo ya kufundishia ya kiutaalamu “

Pia Mahenge alisema Mradi huo umejikita katika utoaji wa vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta lakini pia uunganishwaji wa vyuo hivi 35 katika mkongo wa Taifa wa mtandao.

Mahenge alisema Mradi huo umeweza kujenga chuo kikuu kikubwa Kasuru kilichojikita katika matumizi ya nishati ya kujali mambo ya kimazingira.

“Kutumia nishati mbadala ambapo kuna mtambo mkubwa wa Biogas umejengwa hapo ambao unatumia kinyesi cha binadamu pamoja na mabaki ya chakula ambayo yanatoka baada ya wanafunzi kula na kuyapeleka kwenye Biogas na kuzalisha nishati ambayo inatumika katika kupikia tena”

Naye Mkuu wa chuo cha walimu Morogoro na Mwenyekiti wakuu wa vyuo vya serikali Tanzanzia Bara, Augustino Sahili alisema kupitia mradi huo wa TESP wamenufaika nao hasa katika magunzo kwa kupata mafunzo ya wafanyakazi wote wakiwemo wakufunzi wa vyuo katika masomo yao, mafunzo katika wakufunzi wote katika ICT na mafunzo kwa wafanyakazi wasio wakufunzi katika kada zao mbalimbali.

Pia Sahili alisema wamenufaika na Mradi huo katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu.

“Vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya sayansi vimejengewa maabara mpya na vimejengewa laibrali kubwa na vyuo vyote vimepata ukarabati wa aina mbalimbali”