April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mpango: Dhamira ya Rais Samia ni kulinda Mazingira

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dodoma

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema katika jukumu alilonalo la kuibeba Ajenda ya Nishati safi ya kupikia barani Afrika itawezesha kuhifadhi misitu na kulinda mazingira nchini.

Rais amesema hayo wakati akizungumza kwa njia ya simu na washiriki
wa Kongamano la Wanawake la Nishati Safi ya Kupikia linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.

Amewahimiza wanawake nchini Tanzania kutekeleza yatakayozungumzwa katika kongamano hilo na kuwaahidi serikali itaunga mkono yale yatakayotekelezwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akifungua Kongamano hilo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Philip Mpango, alisema wakati Serikali inakamilisha taratibu za kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi, ni vema wadau mbalimbali kusaidia utekelezaji kupitia mikopo midogomidogo, vikoba au vikundi vya wanawake ili kuhakikisha wanwake wanapata vifaa vya nishati
safi.

Aidha ameitaka Wizara ya Fedha kutazama uwezekano wa kupitia viwango vya kodi kwa majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia ili wananchi waweze kumudu kununua majiko hayo kwa urahisi. Makamu wa Rais amehimiza vijiji na watu binafsi wanaopata mapato kutokana na biashara ya kaboni kutumia mapato hayo kugharamia nishati safi ya kupikia.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa taasisi za utafiti, sekta binafsi na wadau wengine kubuni teknolojia rahisi na zitakazopatikana kwa gharama nafuu ili kuharakisha uhamaji kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu.

Amesema teknolojia zinazohitajika ni pamoja na zile za kupata majiko yanayotumia nishati safi kuwezesha kupika chakula kinachoiva kwa muda mrefu kama maharage na kande badala ya kutumia mkaa au kuni.

Pia ametoa wito kwa sekta binafsi kuunga mkono na kuchangia katika
kampeni ya kuondokana na matumizi ya nishati chafu. Amesema ni muhimu Sekta binafsi kutumia mifuko ya Wajibu kwa Jamii kuwezesha kaya na taasisi zinazowazunguka kupata nishati safi ya kupikia mjini na vijijini.

Makamu wa Rais ametoa wito wadau wote kuandaa programu mbalimbali
zitakazotoa elimu na hamasa kwa jamii nchi nzima ili kuongeza uelewa juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ameviasa vyombo vya habari na Asasi za kiraia kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuwa mstari wa mbele katika kuielezea kwa umma wa Watanzania. Amesema Vyombo vya habari vinao wajibu muhimu wa kuelezea umma kuhusu madhara ya kuendelea kutumia nishati chafu ikiwemo kupoteza misitu, mmomonyoko wa udongo, kuongeza gesijoto, magonjwa ya mfumo wa hewa na madhara ya kiuchumi
kama watoto wa kike kushindwa kumaliza masomo.

Makamu wa Rais amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele cha juu kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia hapa nchini kwenye ajenda ya Taifa ya maendeleo pamoja na kuongeza rasilimali kuhakikisha ajenda hiyo inafanikiwa.

Amesema Rais amefanya maamuzi makubwa ikiwemo kuunda Kamati ya Kitaifa itakayosimamia utekelezaji wa ajenda hiyo, kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi na kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi za Serikali zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku.