May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mollel atoa rai kada ya Uuguzi na Ukunga kujumuishwa kwenye mfumo wa maamuzi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

NAIBU  Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa kada ya Uuguzi imekuwa muhimu katika kutoa huduma bora nchini  sababu asilimia 80 ya kazi za afya zinatekelezwa na kada hiyo ambapo alitoa rai kwa kada hiyo kujumuishwa kwenye mfumo wa utoaji wa maamuzi.

Dkt. Mollel amesema hayo jijini hapa leo  Machi 18, 2024 wakati wa kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa utendaji kazi wa utoaji wa huduma za uuguzi na Ukunga inayokwenda Sanjari na uzinduzi wa jarida la idara ya Uuguzi na Ukunga yanayokwenda na kaulimbiu ya “Huduma staha na Mawasiliano ni wajibu wa kila mtoa huduma za afya”kilichoandaliwa na  Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Amesema kuwa wauguzi na wakunga wanapopata fursa ya kuingia ndani ya mfumo wa uongozi watasaidia kuhakikisha mambo yanaboreshwa kwenye sekta ya Afya lakini pia maslahi yao kwani ndio wamekuwa watendaji wakuu ambao wanakaa muda mwingi na wagonjwa hivyo ni muhimu wakawekwa kwenye mfumo wa uongozi na utoaji wa maamuzi na uundwaji wa sera.

Vilevile amesema kuwa asilimia 60 ya watumishi katika sekta ya afya nchini wanatoka  kada za uuguzi na ukunga hivyo kuchangia ubora wa huduma zinazotolewa katika Hospitali na Vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usajili, Leseni na Maadili kutoka TNMC Jane Mazigo amewataka Wauguzi viongozi kutoka ngazi zote za kutolea huduma za Afya nchini kusimamia vyema huduma za Afya nchini sambamba na kuhakikisha huduma ya Uuguzi na Ukunga zinafuata Maadili, taratibu na miongozo ya huduma ya Afya.

Pia ametaja lengo la kikao hicho kuwa ni kuwaleta pamoja Wauguzi viongozi kutoka ngazi zote za kutolea huduma za Afya chini na wadau mbalimbali wa Afya kujadili na kupanga mikakati ya pamoja ya namna bora ya kuondoa malalamiko kwa wananchi kwa kuhakikisha huduma zinazojali utu, heshima, upendo na mawasiliano madhubuti baina ya mtoa huduma na mteja zinatolewa, pia kuweka mikakati ya kuimarisha usimamizi wa wanafunzi wauguzi katika maeneo ya kutolea huduma za afya.

Naye Mkurugenzi wa idara ya Huduma za Uuguzi na Ukunga  Ziada Sella ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuajiri Wauguzi na Wakunga zaidi ya 40,000 kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 na kuongeza kuwa  kada hiyo ina dhamana kubwa katika utoaji wa huduma hivyo wazingatie miongozo, kanuni na sheria zilizowekwa kwa maslahi ya taifa.

“Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuajiri wauguzi na wakunga zaidi ya elfu arobaini hii inaonyesha umuhimu na dhamana ya kada hii kwa sababu hawa ndio hutumia muda mwingi kukaa na wagonjwa.

Kikao hicho kilichowakutanisha viongozi wa Mikoa, Halmashauri, Hospitali ya Taifa, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali maalum, wauguzi wakufunzi kutoka Vyuo vikuu na Vyuo vya Kati.

Hata hivyo Maratibu wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka OR-TAMISEMI,Jesca Tryphone alitoa rai kwa viongozi hao kwenda kutoa elimu ya usafi na utunzaji wa vifaa kwa wauguzi na wakunga ili kutoa huduma bora na staha kama kauli mbiu inavyosema.