December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Magufuli atolea ufafanuzi bilioni 799.52 za miradi

Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Kigoma

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.John Magufuli amesema takribani Sh.bilioni 799.52 zimetumika katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya miji nane katika Mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza katika Uwanja wa Lake Tanganyika Dkt. Magufuli amesema miongoni mwa miji hiyo ni Arusha, Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwanza, Manispaa ya Ilemela, Mbeya, Tanga, Dodoma na Mji wa Kigoma.

Amesema, kwa Kigoma pekee yake imetengwa kiasi cha Sh. bilioni 31.19 kwa ajili ya kuuendeleza Mji wa Kigoma katika ujenzi wa miradi ya miundombinu ya barabara, mifereji na dampo la kisasa.

“Mkiona mtu anasimama mbele ya wananchi wa Kigoma halafu anasema mradi wa kuuboresha miundombinu ya Mji wa Kigoma amefanya nini maana yake hata Dodoma amepeleka yeye? msema kweli siku zote mpenzi wa Mungu hivyo tujiepushe na matapeli wa kisiasa na kwenye siasa matapeli wapo, ” amesema Dkt. Magufuli.

Utekelezaji wa mradi hiyo ya maendeleo upo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015 na kilichofanyika ni kuendeleza miji hiyo ni utekelezaji wa Ilani hiyo.

Amefafanua kuwa, katika Mji wa Kigoma zimejengwa kilomita 15.13 za barabara za lami wakati kwa Dodoma mradi huo umewezesha kujengwa kwa soko, stendi ya kisasa, na taa za barabarani.

Kuhusu maendeleo yaliyofanyika Mkoa wa Kigoma Dkt. Magufuli amesema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kiasi cha Sh.bilioni 567 zimetumika kwa ajili ya miradi ya barabara.

Amesema, katika kipindi kifupi Kigoma haitakuwa na tatizo la barabara kutokana na fedha hizo kusaidia katika kutengeneza barabara nhivyo wakae mkao wa kutengeneza biashara baada ya barabara kukamilika.

Hata hivyo Dkt.Magufuli amesema, walipoingia madarakani mwaka 2015 walifufua zao la Mchikichi kwa lengo la kuufanya Mkoa wa Kigoma kuwa juu kiuchumi na katika kuhakikisha zao hilo linafufuliwa aliwahi kumtuma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kama hatua ya kufufua zao la mchikichi na kwamba anashangaa kusikia watu wakisema wamefufua zao hilo.

Pi amesema, alipoingia madarakani alisema hawezi kuucha Mkoa wa Kigoma kuwa nyuma kimaendeleo, hivyo alitengeneza mkakati wa kutosha kwa kuteua mawaziri watatu kutoka Mkoa huo na kwamba lengo kuteua mawaziri hao ni kuifanya Kigoma kuwa katika ramani ya nchi.