December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mabula atoa maagizo NHC

Na Munir Shemweta, Masasi

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameliataka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwasiliana na mikoa na halmashauri zilizoko pembezoni ili kujenga nyumba za makazi katika maeneo hayo. 

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo leo Julai 27, 2021 Masasi mkoani Mtwara wakati wa uzinduzi wa nyumba 54 za makazi pamoja na jengo moja la huduma katika eneo la Napupa lilipo wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Amesema, kwa sasa kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali nchini na sehemu mojawapo ya maeneo hayo ni mikoa ya pembezoni na kubainisha kuwa kwa sasa uhitaji wa nyumba za makazi kwa nchi nzima ni takriban nyumba laki mbili kwa mwaka.

“Kuhusu ongezeko la uhitaji wa nyumba za makazi,mikoa mingi iliyo pembezoni ina shida nyumba za makazi na takwimu zinaonesha tunahitaji nyumba za makazi laki mbili kwa mwaka kwa nchi nzima hivyo naielekeza NHC  kuwasiliana na mikoa ya pembezoni kama vile Kigoma na Lindi  ili watumishi wanaopelekwa maeneo hayo kuondoa hofu ya makazi,” amesema Dkt.Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisoma maandishi katika jiwe la msingi akioongozwa na Afisa Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa Domina Rwemanyika baada ya kuweka jiwe la msingi wakati wa uzinduzi wa nyumba 54 za makazi Napupa Masasi mkoa wa Mtwara tarehe 27 Julai 202. Kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Dkt.Maulid Banyani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, Shirika la NHC lilikuwa na changamoto katika ujenzi wa miradi yake ikiwemo halmashauri kushindwa kulipia nyumba ambazo iliomba kujengewa na kubainisha kuwa, kwa sasa halmashauri nyingi zimeamka na kuwa na uhitaji mkubwa wa nyumba za makazi kwa ajili ya watumishi wake.

Amesisitiza kuwa, uhitaji wa nyumba kwa halmashauri katika maeneo mbalimbali ni fursa kwa shirika la Nyumba kuweza katika miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na kuishauri NHC kuwekeza katika halmashauri pamoja na ile mikoa iliyo tayari na kutekeleza miradi ya ujenzi.

Naibu Waziri Mabula alisema, mradi wa nyumba za makazi wa Napupa alioziundua Masasi ni mradi wa tatu kuuzindua akiwa kwenye ziara yake ya kutembelea mikoa mbalimbali nchini na alilipongeza  Shirika la Nyumba na bodi yake kwa kazi nzuri ya utekelezaji miradi ya ujenzi na kuitaka  NHC kuhakikisha miradi hiyo  inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilpnavyotakiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt. Maulid Banyani alieleza kuwa, mbali na shirika lake kutekeleza mradi wa nyumba za makazi wilayani Masasi katika maeneo mbalimbali lakini pia inayo miradi ya jengo la Rahaleo na nyumba za makazi zilizopo eneo la Shangani ikiwa ni mkakati wa shirika kutekeleza miradi ya ujenzi.

Amesema, Shirika la Nyumba litajitahidi kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya ujenzi nchini na kwa mkoa wa Mtwara pekee Shirika limewekeza miradi ya takriban shilingi bilioni 19.2 na kusisitiza kuwa NHC inaendelea kufanya jitihada za kujenga makazi bora.