April 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Kingu mjumbe wa Bodi ya TCCIA

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Binadamu, Said Kingu amechaguliwa kuwa miongoni mwa wa wajumbe nane wa Bodi ya Wakurugenzi ya Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).

Akizungumzia hatua hiyo jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Bodi, Paul Koyi, amesifu uamuzi huo akisema chemba yao kila mara inajitahidi kutumia ujuzi wa wataalamu mbalimbali ili kuendeleza chemba na jumuiya ya biashara nchini Tanzania.

“Tunautafasiri uamuzi huu kama hatua nzuri katika maendeleo ya chemba yetu. Kila mara tunajitahidi kutumia wataalamu wetu kuendeleza chemba yetu na kuinufaisha jumuiya ya biashara nchini,” amesema Koyi ambaye pia ni Rais wa TCCIA.

Dkt.Kingu ameshukuru jumuiya hiyo kwa kumchagua kuwa mjumbe wa bodi na kusema hiyo ni heshima kubwa kwake.

“Nitatumia uwezo wangu na maarifa niliyonayo kutoa mchango stahiki na kuiletea maendeleo chemba yetu na nchi kwa ujumla,” ameahidi Dkt.Kingu na kuongezea kuwa amejiunga na chemba hiyo kwa sababu ya umuhimu wake katika kujenga uchumi wa nchi.

Ameeleza kuwa siku zote anaamini katika kufanyakazi kwa ushirikiano ndio siri ya mafanikio mahali popote na kuongeza kuwa anaamini kuwa mjumbe wa bodi hiyo kutaongeza kasi ya utendaji.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chemba ya Wenye Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Dkt Said Mtemi Kingu akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

“Tanzania ni yetu, mimi ni Mtanzania. Ni lazima niitumikie nchi yangu kwa faida ya yangu na nchi kwa ujumla hivyo kwangu kuwa mjumbe wa bodi ya TCCIA ni sehemu ya kuitumikia nchi. Chemba hii inagusa watu wengi katika nyanja tofauti za kiuchumi,” ameeleza.

Dkt.Kingu ameseama sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa nchi, kwani inatoa ajira nyingi na kuwa kupitia biashara imekuwa ikiingiza fedha ya kigeni ambayo inachochea maendeleo.

“Rai yangu kwa wanataaluma wengine nchini wazione taaluma zao kuwa ni biashara, hivyo wajiunge ma chemba hii ili waweze kupata fursa za kuendeleza biashara zao,” amesema Dkt.Kingu.

Amesema wapo wataalumu ambao wamefungua ofisi za ushauri. Amewashauri wazione ofisi zao kuwa ni biashara kama biashara nyingine na kwamba wana kila sababu ya kujiunga na TCCIA ili waweze kupata mbinu za kuboresha biashara zao, kukuza vipato vyao na kuchangia katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Wajumbe wengine wa bodi ni Njile Bwana, Eutropia James, Judith Karangi amabye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA na Katibu wa Bodi, Dkt.Meshack Kulwa ambaye ni makamu mwenyekit (biashara), Swallah Swallah makamu (kilimo), Clement Bocco makamu (viwanda) mwenyekiti Bw Koyi a mbaye pia ni Rais wa Chemba hiyo.