January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Gwajima afanya mazungumzo na Balozi wa Pakstani nchini Tanzania.

Na.WAMJW- DOM

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo amekutana na Balozi wa Pakstani nchini Tanzania Muhammad Saleem ambapo wamekubaliana kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika uwekezaji na utengenezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.

Dkt. Gwajima amemhakikishia utayari wa Wizara yake kushirikiana zaidi na Ubalozi huo kwa kupeleka wataalam wake Pakstani kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu na mfupi ili kuweza kufikia matokeo chanya ya mapinduzi ya uzalishaji wa dawa nchini .

Naye Balozi Muhammad Saleem amesema Pakstani iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya hususani katika swala la miundombinu, vifaa na kuwekeza viwanda vya dawa nchini Tanzania.

Kikao kimefanyika katika ofisi za Wizara zilizopo Jijini Dodoma, kimehudhuriwa pia na Wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.