Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Inadaiwa kuwa migogoro ya ndoa ni moja ya changamoto inayokwamisha malezi na makuzi bora na kuchangia ongezeko la watoto wa mitaani.
Hivyo wito umetolewa kwa wazazi kuhakikisha wanamaliza migogoro yao ndani bila kuwahusisha watoto,hali ambayo inaelezwa kuweza kujenga chuki.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko,wakati wa maadhimidho ya kitaifa ya siku ya familia na kongamano la malezi kitaifa,lililofanyika mkoani Mwanza,amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kutenga muda wa kujadili changamoto zao za kifamilia bila kuwahusisha watoto.
“Watoto wamekuja duniani sisi tukiwepo, kwa nini tugombane mbele yao,muyamalize wenyewe bila kushirikisha watoto,”amesema Dkt.Biteko.
Dkt.Biteko,amefafanua kuwa mtoto ni zao la matokeo ya upendo baina ya baba na mama,lakini amejikuta akibeba gharama za ugomvi wa wazazi na kujikuta akiangukia mtaani.
“Hakuna mtaa unaozaa mtoto,bali ni watoto wa watu ambao,wazazi wao wameacha wajibu wao kwa namna moja au nyingine wanakosa mahali pa kwenda,na kujikuta anabatizwa mzazi mpya anateitwa mtaa,jambo hilo ni aibu kwa wazazi,”amesema Dkt.Biteko na kuongeza:
“Tusiwe watu wabaya kwa kutelekeza watoto na familia zetu,kwani familia ni msingi wa jamii yoyote,hivyo tustahimiliane,tupendane, tuvumiliane na kuchukuliana madhaifu,”.
Pia ametoa wito kwa wazazi kila mmoja atimize wajibu wake wa kules familia kwa kutenga muda wa kukaa na watoto ili kuweza kuwarithisha mila na desturi tunazo zifahamu.
“Kawaida kwa mzazi kuulizia kama mbuzi wake wameingia bandani lakini aulizi mtoto wake ameshindaje.Ukitaka kuharibu jamii,haribu familia ukitaka kustawisha jamii basi stawisha familia,tuelewe mtoto anapolelewa vizuri tunaandaa jamii ilio bora kwa ajili yetu wenyewe,”.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema kwa mwaka wa fedha 2024–2025, Idara ya Ustawi wa Jamii imepokea mashauri 3,534 ya migogoro ya kifamilia, ikiwemo migogoro ya ndoa 980, ambayo imedaiwa kuwa chanzo cha kukosekana kwa malezi bora ya watoto na kuchangia uwepo wa watoto wa mitaani.
“Tulifanya uchunguzi kwa zaidi ya watoto 1,000 wa mitaani na sababu kuu walizotaja ni migogoro ya ndoa katika familia zao, ambazo zimechangia wao kukimbilia mtaani,”amesema Mtanda.
Pia Mtanda, amesisitiza mafunzo kwa watoto huku akionya kuzaa nje ya ndoa,kwa madai kuwa ni miongoni mwa migogoro inayo kwamisha malezi na makuzi bora kwa mtoto.

More Stories
Mchengerwa afurahishwa na utendaji wa Meya Kumbilamoto
Waziri Lukuvi amuwakilisha Rais Samia Tabora
Thabo Mbeki aipongeza Tanzania kuandaa mhadhara wa UNISA mara tatu mfululizo