May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko: Jitihada zinafayika kupunguza makali ya umeme nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema, Wizara ya Nishati inafanya jitihada mbalimbali ili kupunguza makali ya umeme nchini na kuwaondolea wananchi matatizo hayo.

Dkt. Biteko amesema hayo leo, baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Nyanguku na Bunegezi wilayani Geita, Mkoa wa Geita pia alizungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara katika vijiji hivyo.

“Tumekubaliana, Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi warudi Dodoma kushughulia masuala ya mgawo wa umeme, tunataka tupunguze mgao
huu kwa kasi kubwa ili wananchi wasipate matatizo ya umeme.

“Vilevile Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga anatembelea vituo vya kufua umeme, alianzia Ubungo, ameenda Tegeta na maeneo mengine, lengo letu ni lile, kupunguza makali ya mgawo wa umeme kwa watu wetu,” amesema Dkt. Biteko.

Ameeleza, Wizara ya Nishati inalitekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la
kushughulikia changamoto za upatikanaji umeme wa uhakika ndani ya miezi sita ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila matatizo.

Kuhusu umeme vijijini amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inataka umeme uwafikie wananchi wote na kwa Mkoa wa Geita imetoa shilingi
bilioni 39 kwa ajili ya usambazaji umeme vijijini mkoani humo na dhamira ya Serikali ni kufikisha umeme kaya kwa kaya.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza suala la viongozi kusimamia fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali, wawahudumie wananchi na kuwapa nyenzo za kuwawezesha kufanya kazi ili wajikwamue katika maisha yao.

“Tunachotaka ni kuona kila senti iliyokusudiwa kwa ajili ya miradi inawafikia wananchi, umetaka iwafikie, hutaki mwachie mwingine
anayetaka kuwahudumia wananchi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko (wa Tatu kulia) akiwasha umeme katika Kijiji cha Nyanguku wilayani Geita, Mkoa wa Geita. Wa Tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella.

“Na nyie wananchi miradi ikijengwa kwenye eneo lenu msiiache bali nendeni mkaisimamie kwani tunachotaka kuona hii miradi inamilikiwa na wananchi,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Awali, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, alisema, Mkoa wa Geita una 486 na hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu, REA imeshapeleka umeme kwenye vijiji 359 na vijiji vilivyobaki tayari mkandarasi anaendelea na kazi na ameshaanza kuwasha umeme kwenye vijiji alivyokabidhiwa.

Ameongeza, kwa Wilaya ya Geita Serikali imetoa shilingi Bilioni 2 ili kupeleka umeme kwa vijiji vilivyopo wilayani humo na shilingi
bilioni 6.9 zimetolewa kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vijiji-miji vya wilaya ya Geita.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Biteko (katikati) akikata utepe kuashiria uwashaji umeme katika Kijiji cha Nyanguku wilayani Geita, Mkoa wa Geita.