November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko: Bwawa la Julius Nyerere lipo salama

*Asema limepunguza athari za mafuriko

*Atoa pole kwa waathirika wa mafuriko Rufiji

*Aeleza jitihada za Serikali kwa waathirika

*Azungumzia umuhimu wa Nishati Safi ya Kupikia, Bei ya Gesi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lipo salama kutokana na kujengwa kisayansi na hivyo kuendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 2024 jijini Dodoma, katika mahojiano Mbashara kupitia kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge.

“Bwawa letu lipo salama kwani limejengwa kisayansi, ujazo wake wa maji ni mita za ujazo 183 na kwa takwimu za leo ni mita za ujazo 183.4, huko nyuma maji yalikuwa yakiingia mengi sana kwa kiasi cha mita za ujazo 8400 kwa sekunde hivyo yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa.” Amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, bila ya kuwepo kwa Bwawa hilo athari za mvua zingeanza kuonekana tangu mwezi Oktoba mwaka jana lakini hali hiyo haikutokea mapema kwa sababu maji yalikuwa yakiijazwa katika bwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati na TANESCO ilishabaini uongezekaji wa maji katika mto Rufiji kuanzia mwezi Februari, mwaka huu na tahadhari ilianza kutolewa kuhusu kasi hiyo ya maji ili kuanza kuchukua hatua stahiki.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza jijini Dodoma, leo katika Wiki ya Nishati 2024 wakati akifanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia kipindi cha Jambo Tanzania.

Dkt. Biteko ameeleza kusikitishwa kwake na athari zilizotokea kutokana na mafuriko ambayo yamesababisha athari katika maisha ya watu na mali zao na kueleza kuwa Serikali inafanya kila jitihada kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.

Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini, Dkt. Biteko amesema kuwa, watu wengi bado wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia kama vile mkaa na kuni na wananchi wachache wanatumia gesi na nishati nyingine kama vile umeme.

Ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na kwamba Serikali imepitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni moja ya njia za utekelezaji wa ajenda hiyo ambayo inanadiwa na Kinara wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.

Ameongeza kuwa, katika kutekeleza mpango huo wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshatoa waraka wa kutotumia kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu kuanzia 100 na zaidi kama vile Shule na Magereza.

Kuhusu upatikanaji wa umeme wa uhakika Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa uzalishaji umezidi mahitaji hivyo kinachofanyika sasa ni kuboresha miundombinu ya umeme ikiwemo ya kusafirisha umeme kwani baadhi ya sehemu laini za umeme ni ndefu sana hivyo vitajengwa vituo vya kupoza umeme takriban 83 nchini ili kuondoa athari za watu wengi kutopata umeme pale laini inapopata hitilafu.

Kuhusu Bei ya Gesi amekiri kuwa bei ni kubwa na kueleza kuwa, Serikali inaangalia kwa karibu sana suala hilo ili kuweza kupunguza gharama na hii haiishii kwenye gesi pekee bali kwenye majiko banifu na katika mwaka huu wa fedha Serikali itaanza kutengeneza majiko ya bayogesi kwenye nyumba za wananchi wanaofuga mifugo ili watumie nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.