December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko azindua kiwanda kuweka mifumo upashaji, utunzaji joto mabomba ya EACOP

*Asema Rais Samia anatoa fedha za mradi kwa wakati

*Tanzania yatoa asilimia 87 fedha za utekelezaji EACOP

*Asisitiza kampuni za wazawa kupewa kipaumbele

*Kampuni zilizofanya udanganyifu zafutwa

*Waziri wa Nishati Uganda ampa kongole Rais, Dkt. Samia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezindua Kiwanda cha kuwekea mifumo ya kupasha na kutunza joto katika mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga nchini Tanzania, kupitia Mradi wa Bomba la
Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Akizindua mradi huo katika Kijiji cha Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora, Dkt. Biteko amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP umefikia asilimia 27 ikiwa ni kielelezo cha usimamizi madhubuti wa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ambao wamekuwa vinara katika kuhakikisha mradi unafanyika kwa wakati na viwango vya kimataifa.

Amesema, Rais Samia amesimamia kikamilifu mradi kutoka alipoupokea mwaka 2021 kwa kuhakikisha Serikali inatekeleza majukumu yake ipasavyo, ikiwemo kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa wakati ambapo hadi sasa Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 710 kati ya shilingi Bilioni 820 sawa na asilimia 87 ikiwa ni mchango wake kama Mwanahisa katika mradi wa EACOP.

Amesema, utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri ikiwemo suala la utwaaji wa ardhi ambapo malipo yamefanyika kwa asilimia 99.2, ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhi mafuta Chongoleani Tanga umeshaanza na kufikia asilimia 32 na gati ya kupakia mafuta katika eneo la Chongoloeani umefikia asilimia 36.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameitaka kampuni ya EACOP kuhakikisha inatoa kipaumbele zaidi kwa watanzania katika fursa mbalimbali.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto katika mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga kupitia
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Ruth Nankabirwa na kkulia kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato.

Hata hivyo ametoa onyo kwa kampuni za nje ambazo zinachukua fursa za Watanzania kwa kujifanya ni kampuni za ndani ya nchi ambapo udanganyifu huo wamekuwa wakiufanya kwa kushirikiana na baadhi ya watanzania.

“Kumeanza kutokea mchezo kwa baadhi ya kampuni za nje kwa kushirikiana na baadhi ya Watanzania wanatengeneza kampuni ionekane ni ya kitanzania.

“Tumefanya kazi ya kuzikagua kampuni hizi kwa kutumia EWURA na zile zilizobainika zmefanya udanganyifu tumezifuta ili kampuni za ndani zipate kazi kwanza.

“Fursa hizi zinapokuja lazima ziwafaidishe Watanzania kwanza, kampuni zinazotoa huduma lazima ziwe za kitanzania na hii ni kwa mujibu wa sheria ya nchi,” Amesema Dkt. Biteko.

Vilevile ameitaka kampuni ya EACOP kushirikisha wananchi wanaozunguka mradi huo ili wawe ni sehemu ya mradi na kuwa Walinzi wa mradi husika na kuangalia namna bora ya kuwawezesha ili hata baada ya ujenzi wa mradi kukamilika wananchi wa jamii hizo waendelee na shughuli zao (sustainability empowerment).

Aidha, Amesema Tabora ipo eneo la katikati la utekelezaji wa mradi huo wenye urefu wa kilometa 1443 hivyo waone mradi huo ni wao na watoe ushirikiano kwa wakandarasi na Serikali kwa upande wake itahakikisha wanapata yale yote wanayostahili kutokana na uwepo wa mradi huo ikiwemo huduma za kijamii na fursa za mradi.

Vilevile, ametoa pongezi kwa Serikali ya Uganda kwa kuiona Tanzania kama mdau muhimu kwenye maedeleo ya nchi yao na kwamba Serikali ya Tanzania inatambua mchango huo na kuuthamini.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto katika mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta ghafi
kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Kiwanda kipo Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora

Dkt. Biteko amesema, Serikali ya Tanzania na Uganda zipo kwenye majadiliano ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa Bomba la Gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda ikiwa ni maelekezo ya viongozi Wakuu wa Nchi hivyo Wizara ya Nishati itayasimamia kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema Rais Samia anataka kuwaletea maendeleo Watanzania wote, kuwatoa kwenye umaskini na kuwainua kiuchumi kwa kushirikiana na Sekta binafsi hivyo ni muhimu kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Sekta binafsi na kutowakwamisha.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Ruth Nankabirwa amesema, uzinduzi wa kiwanda hicho ni kielelezo cha hatua kubwa iliyopigwa kwenye utekelezaji wa mradi ambapo ameipongeza kampuni ya EACOP kwa mradi huo ambao umezingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya utekelezaji wa miradi ikiwemo za utunzaji wa mazingira.

Pia, amesema Serikali ya Uganda inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania ili kutekeleza mradi huo kwa ufanisi na kwa wakati.

Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Uganda katika nyanja mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa mradi huo wa EACOP.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akisalimiana na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini
wa Uganda, Ruth Nankabirwa kabla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto katika mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi
Chongoleani Tanga kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Kiwanda kipo Sojo wilayani Nzega mkoani Tabora.

Ameongeza kuwa, shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta nchini Uganda zinaendelea vizuri hali inayoendelea kutoa uhakika katika utekelezaji wa mradi wa EACOP.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato amesema mradi wa EACOP ulikumbwa na changamoto katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake lakini Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni wameusukuma hadi kufikia hatua ya sasa na kueleza kuwa Jumuiya ya Afrika Mahariki inajivunia viongozi hao.

Amesema, Rais Dkt. Samia na Rais Museveni hawachori mistari ya kutenganisha nchi bali kuziunganisha kupitia miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Bomba la EACOP, mradi wa umeme kutoka Masaka Uganda hadi Kagera, Barabara kutoka Masaka Uganda hadi Kagera Tanzania na miradi mingine ya maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya EACOP, Martin Tiffen amesema kiwanda hicho kwa sasa kina mabomba ya mafuta ya urefu wa kilometa 300, huku kazi ya upokeaji wa mabomba mengine kwenye kiwanda hicho ikiendelea hadi kukamilisha kilometa 1,443 za Bomba la Mafuta.
Amesema kiwanda kwa sasa kimetoa ajira 500 huku zaidi ya nusu wakiwa ni Watanzania.

Gharama ya uwekezaji wa kiwanda hicho ni shilingi Trilioni 11 ambapo kiwanda kimeleta faida mbalimbali kwa wakazi wa kijiji cha Sojo na Mkoa wa Tabora kwa ujumla ikiwemo ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, fursa za biashara, uboreshwaji wa barabara, miradi ya kijamii n.k

Baadhi ya mabomba yatakayotumika kwenye mradi wa Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP).

Hafla ya uzinduzi wa kiwanda imeenda pamoja na utiaji saini mkataba kati ya EACOP na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wa kukodisha eneo la kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta mkoani Tanga, mkataba wa kutumia eneo la Maji pamoja na mkataba wa kufanya shughuli bandarini ambao umesainiwa kati ya EACOP na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Viongozi mbalimbali walioambatana na Dkt. Biteko katika uzinduzi huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Fred Mwesigye na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mej.Jen.Paul Kisesa Simuli.