November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko ashiriki Misa Takatifu kumuombea Hayati Magufuli Chato

*Asema Rais, Dkt. Samia anatekeleza kwa kasi kubwa misingi iliyowekwa na Hayati Magufuli

*Dkt. Samia ajenga Makumbusho ya Hayati Magufuli Chato

*Familia ya Magufuli, Mbunge Chato wamshukuru Rais

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo amejumuika na viongozi na wananchi mbalimbali katika misa Takatifu ya kumwombea Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mt. Yohana Maria Muzeyi, wilayani Chato mkoani Geita.

Akitoa Salaam za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Biteko amesema, Dkt. Samia na Serikali yake inaendelea kumkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Magufuli si tu kama Rais katika Serikali Awamu ya Tano, bali pia kama kiongozi aliyeweka misingi mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuitekeleza.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko (kushoto) akitoa heshima katika kaburi la Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya misa Takatifu ya kumwombea Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mt. Yohana Maria Muzeyi, wilayani Chato mkoani Geita. Kushoto kwake ni Mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani.

Ametaja miradi mbalimbali ambayo ilianzishwa katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ni pamoja na mradi wa umeme wa Julius Nyerere ( JNHPP), ambao sasa umeshaanza kuzalisha megawati 235, mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kutoka Dar es Salaam ambao tayari umeshaanza kufanyiwa majaribio na ujenzi wa Daraja kubwa la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza ambao umefikia asilimia 80.

Dkt. Biteko amewahakikishia Watanzania kuwa, masuala yaliyobuniwa na Hayati Magufuli yanaendelea na yataendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na Serikali ya Awamu ya Sita ili kuendelea kumuenzi kwa vitendo.

“Hayati Magufuli anasifika kote duniani kwa uwezo wake wa kiongozi, karama ya kutatua matatizo ya wananchi, kuwasikiliza wananchi, kuondoa kero, uzembe, ubadhirifu, rushwa na kuhimiza uwajibikaji serikalini, nataka niwahakikishie kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayasukuma masuala yote hayo ili kutoa huduma kwa ufanisi kwa watanzania.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Vilevile, amempongeza Mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janet Magufuli kwa kuendelea kusimama kama mhimili wa familia na kuendelea kuunganisha na kuiongoza familia hiyo.

Kwa upande wake, Mjane wa Hayati Magufuli, Mama Janeth Magufuli amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa pamoja na familia hiyo tangu kifo cha Hayati Magufuli ambapo pia amewashukuru viongozi waliojumuika na familia katika adhimisho hilo la misa Takatifu, akieleza kuwa hiyo ni alama ya upendo kwa familia hiyo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko (kushoto) akizungumza na Mjane wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Mama Janeth Magufuli mara baada ya misa Takatifu ya kumwombea Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli iliyofanyika katika Kanisa
Katoliki, Parokia ya Mt. Yohana Maria Muzeyi, wilayani Chato mkoani Geita.

Naye Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali wilaya ya Chato kwani pamoja kuitembelea Chato mara kwa mara, ameendelea kutoa fedha zinazotekeleza miradi mbalimbali kama ya maji, shule, afya ( hospitali ya kanda), barabara n.k

Aidha, amemshukuru Dkt. Samia kwa kuendelea kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna mbalimbali ikiwemo kujenga makumbusho ya Hayati Magufuli wilayani Chato ambayo itafanya historia yake na kazi alizofanya kuendelea kujulikana ndani na nje ya nchi, kizazi cha sasa na cha baadaye

Huu ni mwaka wa Tatu tangu Hayati, Dkt. John Pombe Magufuli afariki dunia tarehe 17 Machi, 2021.

Misa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani.