May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko aendelea na ukaguzi vyanzo vya umeme nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameendelea na ziara ya kukagua vyanzo mbalimbali vya uzalishaji umeme nchini, ambapo leo amekagua Bwala la kuzalisha umeme la Kidatu ( 204 MW) na Kihansi ( 180 MW), mkoani Morogoro.

Lengo la ziara hiyo ni kujihakikisha hali halisi ya uwepo wa maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme nchini, pamoja kukagua mitambo ya kuzalisha umeme.

Mara baada ya kukagua Bwawa la Kidatu na Kihansi pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme, Dkt. Biteko amesema mabwawa ya Mtera, Kihansi na Kidatu yana maji ya kutosha kuweza kuzalisha umeme huku tumaini jingine kubwa likiwa ni umeme kutoka mradi wa Julius Nyerere (JNHPP), ambao muda wowote unatarajia kuingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.

“Nafurahi kuwaambia kwamba changamoto tuliyonayo ya umeme imefika mwishoni, hivyo Watendaji wa TANESCO ni wakati pia wa kushughulikia changamoto nyingine ambazo baadhi ya wananchi wanazipata ikiwemo ya kutotoa huduma kwa wakati na pia ukarabati wa mitambo ufanyike kwa wakati,” Amesema Dkt. Biteko

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekataza Watendaji wa TANESCO kwenda likizo kipindi cha changamoto za umeme na badala yake wajikite katika kutatua changamoto hizo.

Amesema, katika hilo ameagiza Uongozi wa juu wa TANESCO kumchukulia hatua za kinidhamu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro ambaye amechukua likizo katika kipindi hiki ambacho Serikali inapambana kutatua changamoto za umeme.

“Niliposema TANESCO hamtolala kipindi cha mgawo wa umeme nilimaanisha kuwa kila mtu awepo kwenye kituo chake cha kazi, sisi wenyewe tunahangaika kutatua changamoto za umeme halafu baada ya kufika hapa nimeshangazwa kuona Meneja wa Mkoa, ambaye alipaswa kuwepo kituoni wakati wa changamoto amechukua likizo, hivyo nimewaelekeza watendaji wa TANESCO hakuna kwenda likizo kuanzia sasa,” Amesema Dkt. Biteko.

Hata hivyo amesema, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kila rasilimali kwa ajili ya kuwapatia watanzania umeme hivyo viongozi na watendaji wa Wizara hawatakuwa kikwazo cha kumkwamisha.

Ameeleza kuwa, kwa sasa kutakuwa na ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji katika kulinda vyanzo vya maji na kwamba itatengenezwa timu ya pamoja ya Serikali, kuhakikisha kwamba vyanzo vyote vya maji vinavyoleta umeme vinalindwa kwa gharama yoyote na wote wanaovamia vyanzo hivyo watachukuliwa hatua.

Vilevile. Dkt. Biteko ameiagiza TANESCO kuhahakisha kuwa wakazi wanaozunguka Bwawa la Umeme la Kidatu wanapatiwa umeme wa uhakika ili waone faida ya kulitunza bwawa hilo kimazingira na pia kuwa walinzi wa Bwawa hilo.

“Wakazi wa Kilombero walioko karibu na bwawa hili waondolewe kwenye mgao, haiwezekani wao wanalitazama na kulinda bwawa, lakini hawana umeme; amesema Dkt. Biiteko na kuwaelekeza wataalam kuumiza vichwa na kuja na mwarobaini.

Kuhusu suala la maji kukatika kwenye baadhi ya maeneo ambapo Mamlaka za Maji zimekuwa zikisema kwamba sababu ni changamoto ya umeme huku wakati mwingine umeme ukiwepo, Dkt. Biteko ameelekeza kuwa umeme usiwe chanzo cha kujificha kwenye utendaji kazi na kwamba kila mtu ajikite kwenye kutoa huduma bora kwa watanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka watendaji wa Sekta za Nishati na Maji kuacha visingizio wakati wa utendaji kazi na wasizoee shida za wananchi na kuongeza kuwa sekta hizo zinategemeana hivyo ni lazima zishirikiane.

Amesema, Wizara yake kupitia mabonde ya Maji yote 9 watakuwa mstari wa mbele katika kutunza na kulinda rasilimali ya maji.

Ameongeza kuwa, suala la utunzaji na ulindaji wa vyanzo vya maji ni jambo shirikishi hivyo Wizara ya Maji na Wizara nyingine kama Mifugo, Nishati na Mazingira lazima zishikamane kulitekeleza.

Pia, ametaka Maafisa katika Mabonde ya Maji nchini kutokukaa maofisini bali jukumu lao ni kusimamia vyanzo vyote vya maji kwa ukaribu na washirikishe wananchi na viongozi kwenye maeneo wanayosimamia.