May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dhamira ya Samia uwekezaji Bandari,kuipeleka Tanzania kwenye neema

Na Mwandishi Wetu

BANDARI ya Dar es Salaam ni maliasili ambayo Watanzania tumejaliwa na Mwenyezi Mungu. Bandari hiyo ni langu la biashara la nchi zinazotuzunguka.

Bandari hiyo kubwa hapa nchini inatupa wajibu wa kuhudumia nchi jirani wanaoitegemea. Kwa mujibu wa makubaliano wa Umoja wa Mataifa, nchi zenye mlango bahari (Bandari) zina wajibu wa kuhudumia na kuhakikisha ustawi wa nchi zisizo na milango bahari.

Kwa kutambua wajibu huo, Serikali imewekeza sana kwenye kuiunganisha nchi yetu na nchi zinazotuzunguka kupitia barabara, vituo vya utoaji huduma mipakani, reli, usafiri wa majini na imeendelea kuboresha bandari zetu za kwenye maziwa.

Kwa lugha nyepesi bandari ni moja ya kiunganishi muhimu cha kibiashara kati ya nchi yetu mataifa mengine kwa kuwa inahudumia shehena kubwa ya mizigo ya nchi jirani na hata mataifa ya mbali.

Kwa kutambua umuhi wa Bandari hiyo Serikali zote tangu awamu ya kwanza zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali za kuifanyia maboresho ili kuongeza ufanisi.

Pamoja ha hatua hizo, bado bandari hiyo haijawa na ufanisi ambao ulitarajiwa na Serikali. Mifano ya kuthibitisha hilo ipo mingi.

Mfano, kwani kwa miaka sita kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2021/2022 Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) taarifa zinaonesha kwamba haikuweza kukusanya mapato yanayofikia malengo yaliyotarajiwa.

Uchunguzi unaonesha kuwa pamoja na juhudi mbalimbali za Serikali kufanyia maboresho Bandari hiyo, bado bandari hiyo ilishindwa kufikia malengo iliyojiwekea kwa kipindi cha mwaka 2015/16 hadi 2021/22.

Sababu ambazo zinachangia Bandari kutofikia lengo ni pamoja na changamoto zinazoikabili Bandari ya Dar es Salaam.

Changamoto hizo ni pamoja na kutokuwepo kwa Gati za Kutosha, ambapo bandari ya Dar es Salaam kwa sasa ina jumla ya gati 12 za kuhudumia shehena ya magari, mzigo mchanganyiko na makasha pamoja na gati mbili za mafuta na kituo kimoja baharini cha kupokelea shehena ya mafuta.

Kwa mujibu wa watoa habari wetu, gati hizo 12 za Bandari ya Dar es Salaam zina uwezo wa kupokea hadi meli 10 kwa wakati mmoja na wastani wa meli nyingine 16 zikisubiri nangani (outer anchorage) kupatikana kwa nafasi gatini.

“Hali hiyo husababisha kuwa na msongamano mkubwa wa meli nje ya
bandari zikisubiri nafasi ya kuingia bandarini, hivyo bandari yetu kuwa ghali katika gharama za usafirishaji (freight costs) kwa sababu wenye mzigo, hulazimika kulipia pia tozo ya adhabu ya meli kuchelewa gatini (demurage charges) inayotozwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),” kilieleza chanzo chetu na kuongeza;

“Mpango Mkakati wa Tatu wa TPA wa kipindi cha mwaka 2016/17 hadi 2020/21, ulilenga kufanya kuimarisha na kuboresha kina cha gati namba 1 hadi 7 pamoja na ujenzi wa gati ya magari, ujenzi wa gati namba 12-13 na kuchimba pamoja na kutanua lango la kuingia na kugeuzia meli.”

Aidha, kilieleza kuwa katika kipindi hicho, miradi hiyo iliyopangwa haikuweza kutekelezeka kutokana na kukosekana kwa rasilimali fedha za kutosha.

Sababu nyingine zilizokwamisha kutofikiwa lengo ni uhaba wa mitambo ya kisasa. Mtoa habari wetu anasema kutokuwepo kwa mitambo ya kutosha na ya kisasa imekuwa changamoto ya muda mrefu kwa Bandari ya Dar es Salaam.

“Pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali katika kuhakikisha bandari zetu zinakuwa na vifaa vya kutosha, bado kuna uhitaji mkubwa katika kuhakikisha kunakuwepo na mitambo inayotumika kutoa huduma kwa meli na shehena ili kufikia malengo ya utendaji yaliyowekwa ikilinganishwa na bandari nyingine au Kitengo cha Makasha kilichopo Gati Na. 8 -11.

Aidha, imebainika kuwa Bandari ya Dar es Salaam haina mitambo ya kutosha ambayo ingewezesha utoaji huduma kwa tija na kupunguza msongamano wa meli gatini pamoja na nangani.

Baadhi ya Mitambo yenye upungufu mkubwa ni pamoja na Ship
to Shore Gantry Cranes, Rubber Tyred Gantry Crane, Mobile Harbor
Crane, Reach Stackers, Terminal Tractors na Mobile Crane.

Sababu nyingine ni kutokuwepo kwa Mifumo ya Kisasa ya TEHAMA. Shughuli za bandari zinajumuisha huduma kwa meli na shehena mbalimbali ambapo kwa upande wa shehena, TPA hutoa
huduma za kupakua, kupakia, kupokea, kuhifadhi na kukabidhi shehena kwa wateja.

Utoaji wa huduma hizo unaambatana na ushirikishaji wa
wadau mbalimbali wa Serikali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) pamoja na wadau wa Sekta Binafsi wakiwemo
Mawakala wa Meli na Forodha.

Hata hivyo imebainika kuwa, TPA inakosa Mfumo mahsusi wa TEHAMA unaounganisha mifumo mbalimbali ya utoaji wa huduma bandarini (Terminal Operating System and Port Community System) katika kutoa huduma za bandari na kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi.

Ili kuwa na huduma zenye ufanisi kwa wateja ambazo zitapunguza muda wa kutoa huduma bora, unahitajika mfumo mmoja wa kisasa wa TEHAMA utakaoratibu shughuli zote za huduma kwa wadau wa bandari, meli, shehena na utawala.

“Kwa sasa, huduma za bandari nchini zinahusisha wadau wa Serikali na Sekta Binafsi zaidi ya 30 ambao mifumo yao haijaunganika na mifumo ya bandari pamoja na ya forodha,” kilisema chanzo chetu.

Sababu nyingine ni kutofikiwa kwa Viwango vya Kimataifa vya
Huduma za Bandari.

“Bandari ya Dar es Salaam haijafikia viwango vya kimataifa ambavyo
vinaweza kuvutia zaidi meli na shehena kubwa kuhudumiwa na bandari
zetu.

Viwango hivyo vinajumuisha muda wa meli kukaa gatini na kusubiri
nangani ambapo meli hutumia wastani wa siku 9.5 tangu kuingia
bandarini, kupata gati, kupakia/kupakua na kuondoka, muda wa mzigo
kuhudumiwa bandarini hadi kumfikia mteja ambao kwa kasha moja kwa sasa ni wastani wa siku 9.3 na hivyo kuongeza gharama kwa wateja katika kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” kilisema chanzo chetu.

Mathalan, Wastani wa muda wa meli kusubiri nangani kwa Viwango vya
Kimataifa ni siku 4 huku Bandari ya Dar es Salaam hutumia siku 5.
Aidha, Muda wa mzigo kukaa bandarini kimataifa ni siku 2 huku Bandari ya Dar es Salaam ikitumia siku 7.8

Sababu nyingine ni kutokuwepo kwa Maeneo ya Kutosha Ndani na Nje
ya Bandari ya Kuhifadhi Shehena Pamoja na Maegesho ya Meli. Kwa sasa wastani wa meli kwa siku zinazosubiri kuingia bandarini
kuhudumiwa (outer Anchorage) ni meli 16 na wastani wa gati zilizopo kwa sasa kuhudumia meli ni meli 10 kwa wakati mmoja.
Hivyo, kwa kuzingatia ongezeko la shehena na idadi ya meli zinazokuja nchini upo uhitaji mkubwa wa kuongeza maeneo ya bandari kwa ajili ya kuhudumia meli na kuhifadhi shehena ndani na nje ya bandari.

Bahati nzuri Watanzania wengi kama sio wote hawaridhishwi na ufanisi wa bandari, ndiyo maana wanaunga mkono uwekezaji, lakini tulipokuwa tunatofautiana ni makubaliano gani yanahitaji kwa ajili ya kuendeleza Bandari.

Mazungumzo yote Watanzania wanakubalia ipo changamoto pale bandarini, tunatofautiana kwenye kuzitatua.

Wapo wanaoamini sisi wenyewe bila mbia tunaweza kuiendeleza. Hayo ni mawazo mazuri ya kimapinduzi, lakini yapo mbali na uhalisi na njia hiyo itatuchukua muda mrefu kufika, wakati dunia inaenda mbili.

Kwa kutambua hilo, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongozwa na dhamira nzuri,Serikali yake imeamua kuingia mikataba mitatu na kambuni ya DP World ya Dubai kwa ajili ya uendelezaji bandari.

Mikataba hiyo imesainiwa juzi Ikulu, jijini Dodoma, ambapo yaliafikiwa baina ya Serikali na DP World yakitekelezwa, bandari yatu itakuwa na ufanisi wa hali ya juu.

Rais Samia, anasema mikataba mitatu muhimu inayohusu uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya TPA kwa niaba ya Serikali na Kampuni ya DP World ya Dubai imezingatia maoni yote yaliyotolewa, pamoja sheria na taratibu zote kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Aidha, anasisitiza kuwa hakuna mfanyakazi atakayepoteza kazi, awe mwajiriwa wa bandari au wale wanaofanyakazi zao bandarini, wakiwemo wafanyabiashara.

Rais Samia, alitoa kauli hiyo Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma alipokuwa akizungumza mara baada ya kushuhudiwa kusainiwa kwa Mikataba hiyo mitatu.

“Napenda niwahakikishie Watanzania maoni yote yaliyotplewa yamezingatia pamoja sheria na taratibu, zote kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Kinachofanyika ni kuhakikisha bandari yetu inafanyakazi kwenye viwango vinavyokubalika duniani, kukuza biashara na hatimaye mapato ya nchi yetu,” anasema Rais Samia.

Anasema Serikali kwa upande wake ilisikiliza michango na maoni mbalimbali iliyotolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), vyama vya siasa, asasi, wanaharakati huru, vyombo vya habari na pia waliangalia maoni katika mitandao ya kijamii.

“Tumewasikiliza viongozi wetu wa dini na baadhi ya viongozi wetu wastaafu.

Tumefuatilia kwa karibu sana hoja za wabunge wakati wa kujadili na kupitisha Azimia la Bunge la Kuridhia Makubaliano ya Awali ya Ushirikiano katika Uendelezaji wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Mamlaka ya Dubai,” anasema Rais Samia na kuongeza;

“Na tulipokea ushauri wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, kwa uhakika naweza kusema hakuna sauti au kundi ambalo halikusikilizwa ama ilipuuzwa,”

Anasema Serikali iliunda jopo la wataalam , lakini pia wanasiasa na wanasheria waangalie hoja zote zilizotolewa wawaambie ni ipi iigie kwenye mikataba na ipi haina mishiko kwenye mikataba.

Rais Samia alisema kazi hiyo ilifanywa vizuri na baadhi waliopedwa kazi ya uchambuzi kutoka sekta binafsi wale wabobezi wa mambo ya kodi, sheria nao waliingizwa kwenye timu ya majadiliano.

“Kwa hiyo tulifanya uchambuzi wa kina na kwa ujumla na kwa kipekee nashukuru Watanzania wote waliojitokeza kutoa maoni yao juu ya mchakato huo na kutuwezisha kupata nyenzo na miongozo ya kuzingatiwa kwa makini katika majadiliano,” anasema Rais Samia.

Anasema linapokuja jambo geni lazima kutakuwa na maoni tofauti na ni haki yetu na ndiyo demokrasia, watu watoe maoni yao.

Kwa mujibu wa Rais Samia inakuwa ni kazi ya Serikali kubeba maoni na kuyafanyia kazi na wao ndicho walichokifanya.

“Mikataba hii iliyosainiwa imezaliwa kutoka kwenye makubaliano ya awali ya lile dude lililoleta maneno mengi, ndilo lililotoa mikataba hii mitatu kama ambavyo iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema Rais Samia na kuongeza;

Rais Samia, anasema ni lazima kukuza ufanisi wa bandari, iweze kusafirisha mizigo mingi ya biashara. Anasema kwa kuzingatia ukweli huo, busara ziliwaelekeza tupate mwekezaji ambaye tutashirikiana naye kuongeza ufanisi.

Anasema walizingatia kuwa wao sio mlango bahari pekee Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa hiyo Rais Samia alisema maboresho yoyote ya kiutendaji yanayokwenda kufanywa kupitia uwekezaji huo yanaenda kukuzwa biashara ndani na nje na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuna bandari zingine mbali na ya kwetu, hivyo wale wanaotaka mizigo yao ifike haraka wanaweza kuchagua Bandari yoyote mizingo yao ipite na wakaitumia.

Anasema kinachotupa turufu dhidi ya washindani wetu ni mlango wetu wa bahari kuwa na masafa mafupi kuingia kwenye nchi za jirani na tunafikika na nchi nyingi kwa kupitia mpaka mmoja, ikilinganishwa na nchi nyingine na mlango Bahari mingine.

Hata hivyo, anasema ukaribu sio sababu peke yake, kwa sababu tumekuwa nao siku zote, lazima tufanyekazi ya kuongeza ufanisi kwenye bandari yetu, kwani wafanyabiashara uangalia gharama.

Anashukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri wao makini na kuridhia Azimio la makubaliano ya Awali ya Ushirikiano ya Uendeshaji wa Bandari Juni 10, 2023.”

Aidha, analishukuru Baraza la Mawaziri kwa kubariki mikataba hiyo mitatu iliyosainiwa kwa mazingatio ya Kifungu cha Pili cha Sheria ya Ubia No: 6 ya mwaka 2023 na Kifungu cha Pili cha Sheria ya Ununuzi wa Umma No: 5 2023.

Anampongeza Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na wajumbe wa Kamati ya Majadiliano iliyoongozwa na Amza Johari kwa kazi kubwa ambayo wamefanya na wengine.

Anapongeza uongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu na uongozi wa DP World ya Dubai kwa kushiriki bila kuchoka kwenye majadiliano yaliyotufikisha kwenye makubaliano hayo yanayohusu uendelezaji katika bandari ya Dar es Salaam.

Anasema wanawashukuru kwa uelewa wao na umakini waliouonesha katika kipindi chote cha majadiliano.

“Tunafarijika kuwa wameridhia mahitaji na matakwa yetu kama yalivyobainishwa, ambayo yamezingatia matamanio ya wananchi ya Watanzania na maslahi mapana ya nchi yetu,” anasema Rais Samia