May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC.Mpogolo asisitiza umoja na mshikamano kwa Madiwani

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka Madiwani wa Wilaya hiyo, kuwa na umoja na mshikamano ili kuongeza kasi ya maendeleo wilayani humo ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo katika Kata zao.

Hayo yamebainishwa Februari 20, Mwaka huu jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani, kilichoongozwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbi la Moto, wakati wa uwasilishwaji wa mpango wa bajeti zaidi ya bilioni 278 kiasi kitakacho kusanywa na kutumika katika Halmashauri hiyo kwa mwaka 2024/2025, bajeti ambayo imepitishwa.

Mpogolo amesema ni vyema viongozi hao wakaendelea kusimamia misingi ya umoja na mshikamano kwa ajili ya kuwatumikia wana Ilala.

“Ni jambo jema kuona Halmashauri ina uwezo wa kujiongoza na kujisimamia katika shughuli zake za kimaendeleo na hii yote ni kutokana na ushirikiano mzuri, bajeti iliyopita tulikuwa na bilioni 82 ambapo hivi sasa tunaipambania hii,” amesema Mpogolo.

Hata hivyo, amewataka Madiwani hao kujipongeza kwa kazi nzuri ambayo halmashauri yao imeendelea kufanya huku akitolea baadhi ya mifano ya mafanikio katika Wilaya hiyo kuwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato upande wa leseni ya biashara kufikia zaidi ya milioni 500, kodi ya huduma (service Levy), zaidi ya bilioni 2 na ada ya maegesho zaidi ya bilioni 3.

Ameongeza kuwa, katika mfumo wa vyama vingi vya siasa wapo wasiopenda kuona chama kilichopo madarakani kikisemwa vizuri, ambapo aliwasihi kila mmoja kupeleka maendeleo kwa wananchi wake kwani jitihada za mtu au chama huonekana kwenye kazi.

Pia, amewataka Madiwani hao kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kusimamia vizuri miradi ya maendeleo na kuacha tabia ya kuingilia majukumu, huku akitolea mfano wa kutoa tenda kwa wakandarasi wasiyo na vigezo na badala yake waiachie mamlaka husika kwani kufanya hivyo kunasababisha kucheleweshwa kwa maendeleo kutokana na miradi kutokamilika kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura amesema, Halmashauri hiyo imejipanga kutembelea sehemu mbalimbali ili kuweza kuzibaini rasilimali za serikali zilizo chini ya watu binafsi na kuzirudisha.