Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Chunya
WANANCHI wilayani Chunya mkoani Mbeya wameonywa kuacha tabia ya kuwatolea maneno mabaya na kuwanyanyasa watumishi ambao wanaletwa na serikali kufanya kazi katika wilaya hiyo.
Ambao wamekuwa wakiwaambia kuwa si wenyeji wa wilaya hiyo kwa kuwaeleza watumishi hao kuwa ni wa kuja huku wakidai kuwa wataondoka na kuwaacha hapo hapo.
Hayo yamesemwa leo Mei 15,2023 na Mkuu wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya , Mayeka Simon Mayeka wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za kamati na kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa kipindi cha robo ya tatu kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Sapanjo wilayani hapa.
Mayeka amesema kuwa siku za hivi karibuni kumetokea malumbano mabaya eneo la Binti Manyanga kwa Mganga wa Zahanati si kitendo kizuri kabisa kwani hakuna mtumishi aliyejileta katika wilaya hiyo.
Amesema kuwa kuanzia Mkuu wa Wilaya na watumishi wengine hakuna aliyejileta bali serikali imewaleta kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
‘’Nashukuru Mkurugenzi wa Halmashauri umelimaliza na kumhamisha yule kijana lakini kilichokuwa kinafanyika pale ni kwamba wazawa wa eneo lile walikuwa wakitamba kuwa wao ni wazawa na kuwa tukifanya hivi kwa watumishi ni mbaya sana,hakuna mtumishi aliyejileta katika wilaya hii kuanzia Mkuu wa Wilaya bali tumeletwa na serikali kwa ajili ya kuhudumia watu wa Chunya sasa kwa kauli hizi zinazotolewa dhidi ya wananchi zinakatisha tamaa watumishi,”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Pia amesema kuwa kauli hizo za kibaguzi zinazotoka kwa wananchi wa Kata ya Binti Manyanga sio kauli nzuri zinakatisha tamaa watendaji hivyo kila mmoja afanye kazi kwa kuzingatia wajibu wake namna alivyoelekezwa.
“Vitendo vya kibaguzi ambavyo vimekuwa vikifanywa na wananchi wa Binti Manyanga vinakatisha tamaa na jitihada za ufanyaji kazi kwa watumishi, Madiwani msaidie watumishi katika kata zenu kwani wanakumbana na manyanyaso ya maneno ya kibaguzi ambayo hayana afya kwa kwao,”.
Mayeka amesema kuna Mwenyekiti wa Zahanati ya Binti Manyanga yeye ndiye amekuwa kinara wa kuongoza wananchi wake kumkataa mganga huyo,wanatengeneza mazengwe ya kuwaondoa watumishi hivyo mambo hayo sio mazuri.
Huku akisisitiza kuwatendea vema na kuwapa ushirikiano na kama mtumishi amekosea taratibu zipo na zifanyike na kwamba kuna mtumishi mmoja ni tapeli anatapeli watu na ni mwalimu .
“Utumishi mpo na Tume ya Utumishi wa Walimu,nimemuagiza Ofisa Tawala mwalimu aitwe aulizwe shida nini sasa tusaidiane tusiwape mzigo wa majukumu watu wengine maana huyu mwalimu anafahamika kwa utapeli anaofanya kwani hajatapeli mtu mmoja “amesema Mayeka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Diwani wa Kata ya Kiwanja ,Bosco Mwanginde amesema kuwa kufuatia jambo hilo la kunyanyasa watumishi kujitokeza ameahidi kutembelea kata za wilaya hiyo kuzungumza na wananchi,kuthamini watendaji na kuwapa ushirikiano pindi wanapokuwa katika maeneo yao.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato