November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kyerwa aipongeza TANAPA kusaidia wananchi kuwakabili wanyama wakali, waharibifu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MKUU wa Wilaya ya Kyerwa, Zaituni Msofe amelishukuru Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kupitia Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe kwa ushirikiano mkubwa wanaouonyesha pamoja na jitihada kubwa wanazofanya kusaidia wananchi waliopo jirani na hifadhi pindi wanapovamiwa na wanyama wakali na waharibifu.

Aliyasema hayo Mei 21, mwaka huu, katika hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti na vitendea kazi vijana 12 waliohitimu mafunzo ya kujilinda na wanyama wakali katika Chuo cha Pasiansi Jijini Mwanza.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Zaituni Msofe (kushoto), akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu mafunzo ya kujilinda na wanyama wakali waliomaliza katika Chuo cha Pasiansi Jijini Mwanza. Hafla ya kukabidhi vyeti ilifanyika Mei 21 mwaka huu Wilayani Kyerwa. Picha na TANAPA

“Nawashukuru sana Wahifadhi wa Ibanda-Kyerwa na Rumanyika- Karagwe, wamekuwa wepesi sana kuwasaidia wananchi pindi wanapopatwa na kadhia ya kuingiliwa na wanyamapori wakali katika maeneo yao, tumekuwa tukishirikiana vizuri kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.

“Mmeona ni vyema kuwasaidia vijana hawa kupata mafunzo ya kukabiliana na wanyama waharibifu ili waweze kutoa taarifa na huduma mapema kabla Wahifadhi hawajafika, kwa kufanya hivyo kutapunguza uharibifu wa mazao na vifo vya vinavyotokana na wanyamapori hao,” alisema DC Msofe.

Vile vile amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi unaoendelea katika Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyerwa kwa kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo.

“Serikali inatupenda sana wakazi wa Kyerwa, tukipita kule tunaona kuna mambo yanaendelea hasa ujenzi wa lango la kukusanyia mapato pindi watalii wanapoingia (Complex gate), nyumba za watumishi, pia kuboresha mtandao wa barabara, hii itasaidia sana watalii wanapofika kwetu kuweza kupita na kuona wanyama,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Ibanda- Kyerwa na Rumanyika-Karagwe, Afisa Uhifadhi Mwandamizi Goliath Mtawa alisema anaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na uongozi wa vijiji kwa ushirikiano wao na kutoa vijana ili wapate mafunzo yaliyowajengea weledi wa kukabiliana na wanyamapori hao, sanjari na kutoa taarifa za ujangili ndani na pembezoni mwa hifadhi hizo ili kulinda rasilimali kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Muhitimu wa mafunzo hayo, Festo Domitiani kwa niaba ya wahitimu wenzake, ametoa shukrani za dhati kutokana na mafunzo walioyapata na kuomba mafunzo hayo yaendelee kwa vijana zaidi ili kuongeza nguvu kazi na kuimarika kwa utendaji kazi katika vijiji vilivyopo mbali.

Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kujenga makazi au kulima karibu na maeneo ya Hifadhi ili kuepuka hatari zinazoweza kutokea kutokana na wanyama wakali na waharibifu kama Tembo, Nyati, Kiboko na Mamba.