May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kinondoni amuunga mkono M/kiti wa Mtaa  kufanya usafi

Na Agnes Alcardo, Timemajira Online. Dar

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameongoza zoezi la ufanyaji usafi kwenye fukwe za bahari ya Kidimbwi, zilizopo katika Wilaya hiyo, lengo likiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Beach B, Asha George, za kuhamasisha uwekaji mazingira safi katika fukwe hizo ili kuvilinda viumbe vinavyoishi majini.

Mtambule ameongoza zoezi hilo la usafi katika fukwe hizo, Aprili 20,2024, huku akiwataka wakazi wanaoishi katika Wilaya hiyo, kuwa mfano wa kuigwa kwa kujiwekea utaratibu wa kufanya usafi katika fukwe za bahari kila wiki, hususani katika kipindi hiki cha mvua ambacho bahari uchafuka.

” Nitoe wito kwa wakazi wote wa kinondo kuwa mfano wa kuigwa katika utunzani wa mazingira, hili la kufanya usafi katika fukwe za bahari ni zuri mno kwani pia tunavilinda viumbe vya baharini..lakini pia tunatunza mazingira yetu ambayo pia yanatuongezea pato la Taifa letu,” amesema Mtambule.

Pia amesema, kutokuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa masuala ya taka, fukwe nyingi zimekuwa na mazingira machafu kwa sababu ya utupaji taka ovyo huku akiwataka wakazi wa Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo wa mazingira kwa ajili ya kuendeleza zoezi hilo la ufanyaji usafi katika fukwe ili kuyaacha mazingira hayo kuwa safi na kuvilinda viumbe vya baharini.

Aidha ametoa wito kwa wakazi wanaokaa pembezoni mwa bahari, kuwa mfano kwa kuhakikisha wanatunza mazingira ya fukwe ili yawe safi kwa kutotupa taka ovyo na kujijengea utaratibu wa kufanya usafi katika maeneo hayo na kuwataka kuwa wabunifu kwa kuzitumia taka zisizooza zilizo katika mfumo wa plastiki kuzifikisha semehu husika kwa ajili ya kufanyika uzalishaji mpya ili kujiingizia kipato.

Nae Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Beach B, Asha George, amesema lengo la kuhamasika kufanya usafi katika fukwe za bahari ni kuweka mazingira ya bahari safi pamoja na kuvilinda viumbe vya baharini huku akisema kuwa wakazi wa mtaa huo ni wadau wakubwa wa mazingira.

“Natoa rai kwa baadhi ya watu wenye tabia ya kuziba njia za asili za kupitisha maji na kusababisha mafuriko waache mara moja lakini niwaombe vijana kuacha kukaa vijiweni  badala yake watumie fursa ya taka zisizooza kujipatia kipato kama tulivyoambiwa kuwa huwa zinakusanywa na kurudishiwa kiwandani kwa ajili ya uzalishaji mwingine,” amesema Asha.

Mkurugenzi kutoka Umoja wa Mashirika ya Haki za Binadamu Barani Afrika (AHRN), Olivier Muhizi,  amesema, ili kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Rais  Samia za kutunza mazingira na kuwa na Tanzania ya kijani, watahakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu, ambapo kwa kipindi hiki cha miezi mitatu watakuwa wakifanya usafi kila mwezi na baadae kufanya kila wiki.