November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Ilala akabidhi pikipiki 36 kwa Kata za Wilaya hiyo

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar-es-Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo,amekabidhi pikipiki 36 aina ya Honda, zenye thamani ya milioni 103.8 kwa Kata zote za Wilaya ya Ilala.

Zoezi la kukabidhi pikipiki hizo limefanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar-es- Salaam, ambapo Mkuu huyo wa Wilaya amewakabidhi Watendaji wa Kata 36 wa Wilaya ya Ilala huku akiwasisitiza kuzitumia katika malengo yaliyokusudiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akikabidhi pikipiki 36 aina ya Honda, zenye ya mil 103.8 kwa Watendaji Kata Wilaya ya Ilala zitakazo wassidia katika majukumu yao ya kikazi.

Mpogolo amesema, lengo la Serikali kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kutoa pikipiki hizo ni pamoja na utekelezaji wa kilio cha muda mrefu cha Watendaji hao ambao wamekuwa wakilalamikia kutotekeleza majukumu yao kwa ufasaha kwa sababu ya kutokuwa na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na vyombo vya usafiri.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya, amewataka Watendaji hao kuzitumia pikipiki hizo zilizotolewa katika majukumu ya kikazi na si vinginevyo,endapo atabainika Mtendaji aliyefanya kinyume hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake .

“Napenda kumshukuru Mstahiki Meya wa Jiji kwa kazi kubwa ambayo Halmashauri yake inafanya kwanza kwa kufikia lengo la asilimia 101 na leo meweza kununua pikipiki hizi ambazo zimenunuliwa kwa fedha za mapato ya ndani,”amesema na kuongeza kuwa

“Nasisitiza kwa wadada usije ukaenda kumpa pikipiki hii boyfriend au mume wako,kwani wanaume na sisi wakati mwingine ni wajanja tuna maneno mazuri,kwa hiyo muwe makini asije akakulaghai ukampa pikipiki hii akaenda kufanyia bodaboda,”amesema Mpogolo.

Baadhi ya Watendaji Kata wa Wilaya ya Ilala wakikagua Pikipiki zao

Pia Mpogolo amewataka Watendaji kwenda kufanya kazi vizuri pamoja na kukusanya mapato kwa wingi, jambo ambalo amesema linawezekana hususani hivi sasa kwani wamepatiwa vitendea kazi kama pikipiki ambayo itawarahisishia kazi zao.

Akizungumza kwa niaba ya Watendaji wa Kata zote, Mtendaji Kata ya Ukonga, Tatu Nyamoga wanaishukuru serikali kwa uamuzi mzuri wa kuhakikisha ina wajali watumishi wake, huku akidai kuwa uwepo wa pikipiki hizo utasaidia katika suala zima la ukusanyaji mapato kwa wakati na ufanisi.