November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC ataka vitimwendo vikawe msaada kwa watu wenye ulemavu

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Mbeya

MKUU wa wilaya ya Chunya ambaye ni Kaimu mkuu wa wilaya ya Mbeya,Mrakibu Mwandamizi wa jeshi la uhamiaji,Alhaji Mubarak Batenga amewataka wazazi na walezi waliopatiwa msaada wa vitimwendo kwa ajili ya watoto wenye ulemavu kuvitumia kuwapeleka shule badala ya kuendelea kukaa nao ndani ili elimu wanayopata iwe na manufaa katika maisha yako ya badae.

Viti mwendo hivyo vimetolewa na Taasisi ya Tulia Trust kwa wanafunzi wenye ulemavu na watu wazima ili viwe sehemu ya usaidizi badala ya kutegemea ndugu pekee ambao tayari wanakuwa na majukumu mengine ya kufanya.

Alhaji Batenga amesema hayo wakati akikabidhi vitimwendo vinne na madaftari kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu katika kata ya Itezi Jijini Mbeya.

Amesema Tulia Trust imeshasaidia zaidi ya wanafunzi 3000 na vitimwendo 46 na kuomba waliopatiwa msaada kuvitumia vizuri kwa manufaa.

Akielezea zaidi Alhaji Batenga amesema kuwa kwa kitendo cha wenye ulemavu kupatiwa viti mwendo itapunguza idadi ya watu kupungua kumsindikiza mtu pale anapohitaji kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwasababu mtu mmoja anakwenda na watu wawili mpaka watatu na anayesindikiza shughuli za uzalishaji zinasimama pia inasamsaidia kwanza anahitaji kitimwendo hivyo uwepo wa kitimwendo utamsaidia mzazi kufanya shughuli za kiuchumi.

Joshua Mwakanolo ni Ofisa habari na mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust amesema kuwa mpaka sasa wamefikia kata 36 na Mitaa 181 ya Jiji la Mbeya ambapo lengo lilikuwa ni kutimiza ahadi ya mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust Dkt.Tulia Ackson kuweza kuwasaidia madaftari wanafunzi wenye uhitaji na watu wenye ulemavu 46 na wanafunzi 3000 na kwa kata ya Itezi wamekabidhi viti mwendo vinne.

Kwa upande wake Katibu wa siasa na uenezi chama cha mapinduzi kata ya Itezi , Raphael Mwaitege amewataka wanasiasa kuacha kubeza misaada inayotolewa na Dkt.Tulia.

“Unakuta mtu ni mnufaika jioni anakaa kumsema vibaya Dkt.Tulia kuwa hana kazi yeyote huyo mtu lazima apimwe akili,ndugu zangu wananchi tushindane kwa vitendo na Tulia akileta baiskeli za watu wenye ulemavu wewe leta bajaji wakati mwingine mwanasiasa akilemaa na siasa anaweza akawa kichaa”amesema Mwaitege.