Na Omary Mngindo,Timesmajira Online. Chalinze
MAMLAKA ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASA) Chalinze, imewaonya wananchi wanaochangishana fedha kwa ajili ya kuunganishiwa huduma ya maji.
Imeahidi kufikisha maji katika Shule ya Sekondari Talawanda iliyoko Kijiji cha Msigi Kata ya Talawanda Halmashauri ya Chalinze, baada ya kuwepo malalamiko yanayohusiana na kutokuwepo kwa huduma hiyo shuleni hapo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Mamlaka hiyo, Paschal Fumbuka wakati akizungumza na waandishi wahabari ofisini kwake akijibu malaalamiko ya wananchi wa Talawanda, waliolalamikia kukosekana kwa huduma hiyo hali inayosababisha kutumia maji yasiyosafi na salama.
Fumbuka amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya uwepo wa baadhi ya wananchi kuwachangisha wenzao kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo shuleni hapo, hatua ambayo DAWASA imewaonya vikali huku akieleza kuwa serikali, inaendelea na juhudi za kuwaondolea kero hiyo wananchi wake.
“Mamlaka yetu inaendelea na juhudi zake za kuwafikishia huduma hiyo wananchi, hivyo tunawaonya vikali wanaopita mitaani kuhamasisha michango ili kuunganishiwa maji, hususan Talawanda ambapo tayari tumepokea kesi hiyo,” amesema.
Amesema kati ya Mei 10 na 13 mwaka huu, mamlaka hiyo itahakikisha maji yanafika shuleni hapo na kazi ya kufanikisha zoezi hilo linakwenda kwa kasi, huku akiwaomba radhi wananchi hao kwa changamoto hiyo ambayo mamlaka ilikuwa tayari inaifanyia kazi.
Wazazi wa wanafunzi wanaosoma Sekondari ya Talawanda Sekunde Saito, Tausi Mwinyikondo na Mohamed Kiparai wamesema pamoja na kwamba huduma hiyo ipo kijijini hapo, lakini kwenye shule iliyopo mita chache kutoka kijijini hakuna maji, hivyo kusababisha magonjwa ya milipuko.
“Kama mnavyoyaona haya ndiyo maji yanayotumiwa na watoto wetu wanaosoma kwenye shule hii ya Talawanda ni maji hatarishi kwa afya zao na mara kadhaa, wanafunzi wamekuwa wakiugua magonjwa ya mlipuko kutokana na haya maji,” amesema Tausi.
Nao Saito na Kiparai, wameelezea kusikitishwa kwao kutokana na kutakiwa kuchangishana kiasi cha sh. milioni 10, ili kufikisha maji shuleni hapo kwa lengo la kuondokana na changamoto iliyopo.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi