May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRDB yakabidhi zawadi washindi wa Simbanking

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WATEJA watatu wa Benki ya CRDB leo wamekabidhiwa zawadi zao baada ya
kuibuka washindi kutokana na kufanya miamala mingi ya huduma za benki
kupitia simu zao za mkononi maarufu kama Simbanking.

Akikabidhi zawadi hizo jijini hapa, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi
wa Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema huu ni mwanzo tu kwa wateja wa
benki hii kujinyakulia zawadi katika promosheni ya mwaka mzima ya
Benki ni Simbanking yenye kaulimbiu ya Swahiba – lako, langu.

Adili amesema teknolojia imerahisisha mambo mengi hivi sasa kwa
kuwawezesha wateja kupata huduma kupitia majukwaa tofauti zikiwamo
simu za mkononi ambazo kwa Benki ya CRDB wanayo Programu ya Simbaking
inayowaruhusu kupata zaidi ya asilimia 95 ya huduma zake mahali popote
walipo.

“Simbanking imedumu sokoni kwa zaidi ya miaka 15 sasa, ni njia rahisi
ya kupata huduma za Benki ya CRDB na kwa sasa tunayo kampeni ya
kuwahamasisha wateja wetu na wananchi kwa ujumla kuitumia na wale
wanaoitumia zaidi tunawapa zawadi za aina tofauti. Leo tupo hapa
Chanika kukabidhi bajaji moja na pikipiki kwa washindi wetu
waliopatikana katika droo ya kwanza ya kila mwezi,” amesema Adili.

Waliokabidhiwa zawadi hizo ni Adam Salehe Rashid aliyejishindia bajaji
pamoja na Kibwana Hussein Killongo na Rahma Abdul Kyalumbika
walioshinda pikipiki kila mmoja. Kukabidhiwa kwa zawadi hizo
kunawakumbusha wateja wengine wa Benki ya CRDB kuendelea kutumia
Simbanking hali itakayowaweka kwenye nafasi ya kushinda pikipiki au
bajaji nyingine zitakazokuwa zinatolewa kila mwezi au Toyota Dualis
itakayoshindaniwa kila baada ya miezi mitatu.

“Washindi hawa watatu wa kwanza wamefungua pazia kwa mwaka huu. Naomba
mfahamu kwamba kuna magari manne aina ya Toyota Dualis yanayoendelea
kushindaniwa hivyo nawasihi wateja wetu na Watanzania ambao hawatumii
huduma zetu basi wafungue akaunti kwani kwa kufanya hivyo tu watakuwa
wanaingia kwenye droo ya kushinda moja kati ya zawadi nyingi
tulizonazo,” amesema Adili.

Ili kushinda moja ya zawadi zinazotolewa na Benki ya CRDB, mteja
anatakiwa kufanya miamala mingi kupitia Simbanking kama vile kulipia
bili za umeme na maji, kukata tiketi ya usafiri wa ndege, kulipa ada
na michango ya shule, kulipia bidhaa zinazouzwa mtandaoni au kununua
muda wa maongezi na huduma nyingine nyingi zinazopatikana ndani ya
Programu ya Simbanking.

“Sifa zilizowapa ushindi wateja hawa watatu zinawezekana kwa mteja
mwingine yeyote wa Benki ya CRDB hivyo niwahimize wateja wetu wote
kutoka mahali popote walipo kuendelea kutumia huduma za Simbanking ili
kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda zawadi kemkem tulizonazo,”
amesema mkuu huyo.

Akipokea pikipiki yake, Rahma amesema ataifanya bodaboda ili
imwingizie kipato. “Naamini haitonifaidisha peke yangu. Dereva
atakayekuwa anaiendesha naye atapata kitu cha kuisaidia familia yake.
Nimefurahi kushinda na naipenda zaidi Benki ya CRDB kwani inarudisha
sehemu ya faida yake kwetu,” amesema.

Pichani ni Adam Salehe Rashid mshindi wa bajaji akionyesha funguobaada ya kukabidhiwa zawadi hiyo na Mkuu wa Kitengo cha WatejaBinafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili (wa pili kulia). Adamameshinda bajaji hiyo katika droo ya kwanza ya kampeni ya Benki niSimbanking inayoendeshwa na Benki ya CRDB. Katika droo hiyo, KibwanaHussein Killongo na Rahma Abdul Kyalumbika wameshinda pikipiki kilammoja. Zawadi hizo zilikabidhiwa katika eneo la Chanika jijini Dar esSalaam. (Na Mpigapicha Wetu)