December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Coca-Cola yakusanya maelfu kuona Kombe la Dunia

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MAELFU ya Watanzania, jana wamejitokeza kwa wingi kushuhudia na kupiga picha na Kombe Halisi la Dunia la FIFA lililoletwa nchini ya Kampuni ya Coca-Cola Tanzania, hafla iliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikipambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, na uoneshwaji wa Filamu ya Royal Tour.

Kombe la Dunia lilitua nchini alfajiri ya Mei 31, ambapo lilipokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, kabla ya jana kupelekekwa Uwanja wa Mkapa kuruhusu Watanzania kupiga nalo picha, dhifa hiyo ikipambwa na wasanii mbalimbali wa kizazi kipya, wakiwemo Chegge Chigunda na Mr Bluu.

Wakali wengine waliopamba masaa siya ya hafla hiyo ni Mzee wa Bwax, Sholo Mwamba, Juma Nature na Kala Pina, ambao walikuwa ni miongoni mwa wasanii waliotumbuiza, kuhitimisha siku mbili za Ziara ya Kombe la Dunia nchini Tanzania, iliyofanyika kwa udhamini wa Kampuni ya Coca-Cola Tanzania.

Aidha, Serikali imeipongeza Coca-Cola Tanzania kwa kufanikisha ujio wa ziara ya Kombe Halisi la Dunia la FIFA, huku ikiahidi wa kuitumia ziara hiyo kama chachu ya uboreshaji miundombinu ya soka, ili sio tu kuiwezesha Tanzania kuomba uenyeji wa AFCON 2027, bali pia kuharakisha ukuzaji vipaji vya mchezo huo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, wakati wa hafla ya Chakula cha Usiku cha Waalikwa Maalum wa Ziara ya Kombe la Dunia (FIFA Trophy Tour Night Gala), iliyofanyika jijini Dar es Salaam Mei 31 usiku, ikihudhuriwa na zaidi ya watu 300 walioalikwa na Coca-Cola Tanzania.

Naibu Waziri Gekul alibainisha kuwa, Kampuni ya Coca-Cola na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), limewashika mkono Watanzania, ambao wanapaswa kusapoti jitihada za Serikali yao katika kufanikisha kasi ya ukuaji na uendelezaji wa vipaji nchini, sambamba na ujenzi wa miundombinu inayokidhi viwango vya kimataifa

“Rais Samia Suluhu Hassan ametamka mchana wakati ziara hii ilipofanyika Ikulu, Waziri naye akakazia, nami niseme hapa hadharani kwamba, thamani hii tuliyopewa na Coca Cola Tanzania na FIFA, ya kuwa moja kati ya mataifa manne yasiyofuzu fainali za Qatar kutembelewa na kombe hili, tunapaswa kuienzi kwa vitendo.

“Watanzania wawe na imani na Serikali, Wizara na mipango chanya ya Rais Samia katika Sekta ya Michezo. Tuko kazini kuhakikisha mipango hii endelevu ya kustawisha soka letu, inatekelezeka na kuzaa matunda. Tuwahakikishie kuwa yaliyotamkwa yako kwenye utekelezaji na hivyo Watanzania wajue tuna kazi ya kufanya.

“Kama Serikali tunatumia chachu hii iliyoletwa na Coca-Cola, kuhakikisha tunapita mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, kata ama kijiji kwa kijiji, mtaa kwa mtaa kustawisha soka, ili miaka michache ijayo tusiwe miongoni mwa nchi zinazoletewa kombe hili zikiwa hazijafuzu fainali, bali lije tukiwa na tiketi yetu mikononi,” alisisitiza Gekul.

Naye Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko wa Coca-Cola Afrika, Nelly Wainaina, alisema wao kama Coca-Cola Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, wanajisikia furaha nchi zao mbili za Kenya na Tanzania kuwa mwenyeji wa ziara hiyo, ambayo Watanzania wanapaswa kuitumia kuamsha ari, kiu na hamasa ya maendeleo ya soka.

Aliushukuru msafara wa FIFA ulioongozwa na Juliano Belleti kwa kutua nchini salama na taji hilo, huku akizishukuru kampuni washirika wa Coca-Cola zikiwemo Nyanza Bottlers, Bonite Bottlers na kampuni zingine zinazoidhamini FIFA kwa kuwa sehemu muhimu ya ziara na kuhudhuria hafla hiyo usiku wa juzi.

Awali, mchana wakati wa hafla ya utambulisho wa ziara na taji la Dunia la FIFA kwa wanahabari, Meneja Mkuu wa Biashara wa Coca-Cola Tanzania, Hellen Masumba, wanayo furaha kubwa kuwa sehemu ya kuwaletea Watanzania msisimko na shamrashamra za Kombe la Dunia.

“Kwa miaka mingi Coca-Cola wamekuwa washirika wa FIFA katika kuwapatia msisimko halisi kupitia Ziara ya Kombe la Dunia la FIFA. Kuwasili kwa kombe bila shaka ni fursa ya aina yake kwa Watanzania kujumuika na dunia nzima kupitia ulimwengu wa mpira wa miguu ambapo watawazeza kuliona kwa ukaribu zaidi.

“Ushirikiano wetu na FIFA katika kulileta kombe hili maarufu, ni ishara kwamba tunatambua na kuthamini kile wanachokiamini na kukipenda kwa dhati wateja na watumiaji wa bidhaa zetu hususani mchezo wa mpira wa miguu,” alisisitiza Hellen kwa kuwakaribisha Watanzania jana katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa.

Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Brazir aliyewahi kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2002, Juliano Balletti (kushoto) akisalimiana na mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars Salum Abubakar (Sure Boy) wakati alipowatembelea katika kambi yao ya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, jana.
Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Brazir aliyewahi kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2002, Juliano Balletti, akisalimiana na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, wakati alipowatembelea katika kambi yao ya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, jana.
Mchezaji wa Timu ya Taifa ya Brazir aliyewahi kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2002, Juliano Balletti, akisubiri kupokea pasi kutoka kwa Meneja Masoko wa Cocacola Tanzania, Kabula Nshimbo, wakati walipokuwa wakicheza mpira walipowatembelea katika kambi ya mazoezi ya timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, jana.
Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko wa Coca-Cola Afrika Silke Buker (kulia) akiwa kwenye picha ya Pamoja na Meneja Mwandamizi wa Masoko, Coca-Cola Tanzania Kabula Nshimo (katikati) na Mkurugenzi Mkuu Mwandamizi wa Masoko, Coca-Cola Africa Nelly Wainana wakati wa hafla ya ziara ya Kombe la Dunia Tanzania.