May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chuo cha uuguzi na ukunga Peramiho kufungiwa mtambo wa kupikia wa Gesi wa Tani moja

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameahidi kufunga mtambo wa gesi wa Tani moja katika  Chuo cha Ukunga na Uuguzi cha Peramiho wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa chuo hicho kitakuwa cha  mfano kitakachofanyiwa tathmini kabla ya Serikali kuanza kutoa ruzuku kwa Taasisi kama hizo zitakazofunga mifumo ya gesi ya kupikia.

Waziri wa Nishati, alitoa ahadi  tarehe 31 Julai, 2022 baada ya kukagua mfumo wanaotumia wa kupikia kwa  kutumia magome ya miti ambao una changamoto mbalimbali ikiwemo kuleta moshi mwingi na muda mwingine inasababisha wanafunzi takriban 170 kuchelewa kupata huduma ya chakula

Waziri wa Nishati amesema kuwa ” kama mnavyofahamu kuwa tunatoa mitungi ya gesi kwa makundi mbalimbali vijijini lakini pia kufunga mifumo ya kupikia ya gesi katika taasisi mbalimbali, lengo letu ni kuwaondelea wananchi adha ya kupika kwa kutumia kuni na mkaa, na huu ni utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015.”

Amesema shule hiyo itafungiwa mfumo wa kupikia ambao utajumuisha mtungi wa gesi wa tani moja nje pamoja na mabomba na mfumo wa kupikia  wenye majiko makubwa matatu na sufuria zake za kupikia kubwa zenye uwezo wa kuhudumia watu 200.

Amesema kuwa, kufungwa kwa mifumo ya gesi katika chuo hicho kutawezesha Serikali  kupata taarifa sahihi na kujifunza jinsi Taasisi zinavyoweza kumudu na kutumia mifumo hiyo ya kupikia na kwamba shule hiyo itakuwa ni mfano wa mabadiliko kutoka nishati chafu ya kupikia kwenda nishati safi.

Mkuu wa Chuo hicho cha uuguzi cha Peramiho, Sista Evodia Ngonyani alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kutembelea chuo hicho na kuona jinsi wanavyopika katika mazingira ambayo si salama kutokana na wapishi muda wote kuwa katika mazingira ya moshi ambao ni hatari katika  mfumo wa upumuaji.

Ameongeza kuwa, mtambo huo wa gesi utarahisisha shughuli za upishi na kuepusha changamoto ya wanafunzi kucheleweshewa chakula pamoja na pia kuwezesha chuo hicho kuwa na mazingira safi na salama ya kupikia.