May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chanjo ya Uviko-19,imesaidia kurejesha uchumi wa makondakta na Wasaidizi wake Jijini Mwanza

-Katika mlipuko wa ugonjwa wa uviko-19,uchumi wao uliyumba
-Hofu ilitawala katika utendaji kazi wao
–Wahamasisha wengine kupata chanjo hiyo

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto zikizowakuta makondakta na wasaidizi wao (wapiga debe), jijini Mwanza kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa uviko-19 ni pamoja na kuyumba kiuchumi na hofu.

Hiyo ni kutokana na serikali kutoa maelekezo kwa vyombo vya usafiri hususani daladala kuhakikisha abiria wanakaa kwenye siti kwa kuachiana nafasi( level seat) ili kuepuka msongamano ndani ya gari.

Hivyo baada ya serikali kuruhusu uchanjaji wa chanjo ya uviko-19 ambayo ni moja ya njia ya kupambana na Uviko-19 hali ya uchumi imerejea kama awali kwa kundi hilo.

Akizungumza na Timesmajira ofisini kwao jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Umoja wa Makondakta wa Daladala na Wasaidizi wake(UVDS)Mkoa wa Mwanza Mrimi Juma, hali hiyo iliochangia kwanza kuwa na hofu ukizingatia kazi yao inamuingiliano wa watu tofauti tofauti humu kiuchumi waliyumba kutokana na kipato chao kupungua.

“Kwa kipindi hicho abiria walikuwa wanapatikana asubuhi na jioni….,mchana ukizingatia level seat unakuta gari lenye viti 16 unakuta limebeba abiria 6 na lenye uwezo wa kubeba abiria 36 unakuta abiria 20 tu,jioni abiria unaweza kukuta wengi lakini tulipaswa kuzingatia abiria kukaa kwa kuachiana nafasi hali iliopelekea kushuka kwa mapato ukizingatia mwenyewe gari naye anahitaji hesabu zake,”ameeleza Mrimi.

Mrimi,ameeleza kuwa lilipokuja suala la watu kuchanjwa chanjo ya uviko-19,walikuwa mstari wa mbele kupata chanjo hiyo kwa sababu kutokana na mazingira ya kazi yao stendi ina watu wengi sana, wageni na wenyeji ambao wengi wanatumia daladala kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika mazingira ya Mkoa.

“Tulihamasishana sisi wenyewe kupata chanjo ya uviko-19 ili kuendelea kufanya kazi bila hofu,ukiwa kiongozi lazima uwe mstari wa mbele nilichanja kiukweli baada ya kupata chanjo hizo hatujaona mabadiliko yoyote wala kuona mwanachama amelalamika na kupelekea hospitali kuwa amepata madhara kutokana na chanjo hizo,hofu imeondoka na kipato kimeongezeka,wito makondakta na watanzania kuendelea kujitokeza kuchanja chanjo hiyo kwa sababu ya kujilinda,”.

Mmoja wa makondakta na wapiga debe jijini Mwanza, Sadick Yahaya, ameeleza kuwa kabla ya chanjo ya uviko-19 kuruhusiwa nchini walikuwa wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo abiria kukataa wasiguswe wala kuwashika na ukizingatia shughuli zao katika kumshawishi mtu apande gari fulani kuna muda ulazimika kuwashika mkono.

Yahaya ameeleza, changamoto nyingine ni kushuka kiuchumi kwa sababu daladala hazikupaswa kujaza isipokuwa abiria kukaa kwa kuachiana nafasi pamoja na kujawa na hofu.

Hivyo ameeleza kuwa,alichanja chanjo ya uviko-19 aina ya JJ baada ya mama yake kumshawishi na kumueleza umuhimu wa chanjo hiyo endapo akipata maradhi hayo hatoweza kupata madhara kama mtu ambaye hajachanjwa.

“Kiukweli kiuchumi tuliyumba kwa sababu hata Askari wa usalama barabarani wakikukuta umesimamisha ata abiria wawili anakutoza faini…… nimeisha chanja sina hofu na baada ya chanjo hii kuruhusiwa hali ya kiuchumi kwetu imerejea kama awali kabla ya mlipuko wa ugonjwa wa uviko-19,”ameeleza Yahaya.

Kondakta wa daladala jijini Mwanza Dossa Mashaka, ameeleza walikuwa na hofu katika utendaji kazi wao kwani ni ugonjwa ambao huwezi kujua yupi anao yupi hana ,hivyo watanzania wasisite kupata chanjo hiyo.

“Nilichanja chanjo ya uviko-19 mara mbili ili kujikinga na kuwa na amani katika kufanya shughuli zangu ambayo inamuingiliano wa watu kuingia na kutoka siwezi kufahamu ambaye ameathirika na uviko-19 na yupi hajaathirika hivyo ni vyema nilivyopota chanjo hii imenifanya iendelee kufanya kazi vizuri,”ameeleza Mashala.

Hata hivyo hivi karibuni Julai 2022 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imelenga kufikia asilimia 70 ya watu waliochanja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Dunia wa kupambana dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Ameeleza kuwa Tanzania ikiwa ni mwanachama wa shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa mataifa inaungana na mataifa yote ulimwenguni kuweza kupata kinga ya jamii dhidi ya Uviko-19 kwa angalau asilimia 70 ya watu wote duniani na hadi kufikia Julai 5,2022 Tanzania imefanikiwa kuchanja watu milioni 8.5

Mwenyekiti wa Umoja wa Makondakta wa Daladala na Wasaidizi wake(UVDS)Mkoa wa Mwanza Mrimi Juma akizungumza na Timesmajira online ofisini kwake jijini Mwanza.( Picha na Judith Ferdinand)