April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chuo cha Ualimu Kabanga chajengwa upya, Dkt. Mpango aweka jiwe la msingi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Kigoma

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema ujenzi wa majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga ni moja ya mikakati ya Serikali kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu ya nchini.

Ameyasema hayo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wakati wa kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa majengo mapya ya Chuo hicho ambapo amewataka walimu tarajali kusoma kwa bidii kwa kuwa sasa miundombinu imeboreshwa.

Kiongozi huyo amesema ameridhishwa na taarifa za ujenzi huo kwa kuwa umezingatia matumizi bora ya nishati mbadala na nafuu na pia uhifadhi wa mazingira.

Aidha amesema ni vizuri chuo hicho kikachukua tahadhari zote za kuzuia majanga yakiwemo ya moto na kuwataka walimu tarajali wa Chuo cha Ualimu Kabanga watakaohamia katika majengo mapya ya Chuo hicho kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.

Pia ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuwezesha ujenzi wa majengo hayo mapya ya Chuo cha Ualimu na Vyuo vingine vya Ualimu nchini.

“Serikali ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan inathamini urafiki wa muda mrefu na ndugu zetu wa Canada, nakuomba Balozi kupitia kwako utupelekee salamu zetu kwa Waziri Mkuu wa Canada kutoka kwa Watanzania, tunaishukuru Serikali yake pamoja na wananchi kwa kuendelea kushirikiana nasi tunapofanya jitihada za kujikomboa kielimu na katika maeneo mengine ya nchi yetu Canada imekuwa mbia muhimu,” amesema Makamu wa Rais

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Mradi huo mpaka utakapokamilika utagharimu zaidi ya sh. Bilioni 11 na kwamba umefadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Programu ya Kuimarisha Elimu ya Ualimu (TESP).

Profesa Ndalichako amesema mradi huo utakapokamilika utaongeza idadi ya Wanachuo kutoka 400 hadi 800 na utakuwa na miundombinu yote na vifaa vyote vya kufundishia na kujifunzia.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Sekta ya Elimu, Serikali ya Canada imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali na kushirikiana nao kwenye masuala yanayohitaji ushauri wa kitaalamu hususani kwenye mambo ya elimu ya ualimu ambapo programu ya TESP ambayo ni ya Miaka 7 ina thamani ya jumla ya dola za Canada milioni 53 ambazo ni sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 90 za Tanzania.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiweka jiwe la Msingi katika majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Kabanga-Kasulu, Kigoma. Kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Pamela O’donnel.

Naye balozi wa Canada nchini Tanzania Pamela O’donnel amesema Canada inayofuraha kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika juhudi za kuboresha mfumo wa ufundishaji kwa faida ya watoto wa Kitanzania

Amesema ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga ni wa kisasa unaozingatia mbinu za kimazingira na hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kuchangia juhudi za Serikali za kukabiliana changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Pia itachangia jitihada za maendeleo endelevu ambayo ni nishati safi usawa wa kijinsi na kupambana na madiliko ya tabia nchi na hivyo kukifanya Chuo hicho kuwa cha karne.

Balozi O’dennel ameongeza Canada ni moja ya nchi ya kwanza duniani kupitisha sera ya nchi yenye kuzingatia usawa wa kijinsia na kwamba anafarijika kuona mradi unahakikisha wakufunzi wasimamizi wa elimu na mifumo yote inazingatia usawa wa kijinsia na kwamba Serikali yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha Sekta ya Elimu Hususan Elimu ya Ualimu.