December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR), kt.Jeremia Ponera (kulia) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jijini Dar es salaam, kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa kituo hicho ikiwemo kujitanua na kuwafikia watanzania wengi zaidi sambamba na kuongeza programu na kozi mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025.

Chuo cha Diplomasia chataka vyuo vishirikiane kufaidi diplomasia ya uchumi

Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR) kimependekeza vyuo vishirikiane ili Tanzania inufaike na diplomasia ya chumi ambayo ndiyo chagizo la dunia katika kipindi hiki.

Akizungumza kwenye hafla iliyojadili mwelekeo wa dunia kiuchumi jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa chuo hicho, Dkt. Jeremia Ponera, amesema chuo chao kinatoa mafunzo ya ngazi mbalimbali katika masuala ya uchumi, biashara na uhusiano wa kimataifa na amewataka Watanzania kutumia fursa ya kuwepo mafunzo hayo.

Wakati huu ambao dunia nzima inazungumzia diplomasia ya uchumi, itakuwa haina maana sana ikiwa Watanzania hatutaitafsiri dhana hiyo kwa vitendo. Nawaomba Watanzania wajiunge na kozi fupi na za muda mrefu ili kujitengenezea uwezo kushindani na mataifa mengine, amesema Dkt. Ponera.

Dkt. Ponera amesema wamezifanyia marekebisho kozi ili kukidhi mahitaji ya kiushindani katika biashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda.

Chuo hiki kinaenda sambamba na mipango na mikakati ya serikali na mabadiliko ya kimataifa kibiashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda ambao ndio azma ya Serikali ya awamu ya tano.

Wafanyabiashara wajitokeze kukidhi viwango vya biashara ya kimataifa pamoja na kuwa na ufahamu mpana wa lugha mbali mbali ambazo zitawasaidia kurahisisha biashara zao, ameeleza Dkt. Ponera.

Aidha amezitaka taasisi za umma kuwasiliana na chuo ili kuangalia namna wanavyoweza kuunganisha nguvu katika kuitafsiri dhana ya diplomasia ya uchumi na namna inavyoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

Zipo taasisi na vyuo mbalimbali hapa nchini ambavyo tukiungana navyo tunaweza kuitafsiri vyema dhana ya diplomasia ya uchumi na hata namna ya kushughulikia migogoro katika nchi za Maziwa Makuu ambayo imekuwa kikwazo kwa ukuaji wa uchumi, amesema na kuongeza kuwa tayari chuo chao kinashirikiana na Chuo Kikuu Huria katika utoaji wa kozi ya amani na utatuzi wa migogoro (peace and conflict management)

Amesema CFR ni chuo cha umma licha ya kuwa ni taasisi ya ubia kati ya Tanzania na Msumbiji tangu kuanzishwa kwake mwaka 1978.

“Jambo muhimu la kusisitiza kwa Watanzania ni kuwa chuo hiki ni cha umma licha ya ubia uliopo na jirani zetu Msumbiji na kinakaribisha watu wote kwa sifa za kuanzia darasa la saba, kidato cha nne na cha sita. Kwa hiyo nawaomb Watanzania wajitokeze na kupata mafunzo yanayotolewa hapa,” amesema.

Chuo kinakusudia kujenga matawi katika Jiji la Dodoma, Arusha pamoja na Zanzibar .

Kituo hicho kimejipanga kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya ujezi wa uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.