May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chongolo: Rais Samia anatekeleza Ilani ya CCM

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020- 2025, hivyo wale wote wanaopinga uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam, wanataka kuikwamisha CCM na Serikali yake.

Amesema serikali inatekeleza miradi mingi na Rais Dkt. Samia amekuwa akitekeleza miradi iliyomo kwenye Ilani ya CCM ikiwemo iliyoanzishwa na mtangulizi wake Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Magufuli kama Daraja la Kigongo- Busisi mkoani Mwanza,mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere na reli ya kisasa SGR, lakini hayo yote hawasemi.

Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo akizungumza na kadamnasi mjini Korogwe.

Chingolo amesema hayo Julai 19, 2023 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Mazoezi mjini Korogwe na kuhudhuriwa na wanaCCM kutoka wilaya nane na majimbo 12 ya Mkoa wa Tanga wakiwemo pia madiwani na baadhi ya wabunge wa mkoa huo.

Chongolo amesema kuwa mjadala unaoendelea kuhusu uwekezaji na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam unaotarajiwa kufanywa na kampuni ya DP World kutoka Dubai ni vita ya kiuchumi duniani.

Amesema kuwa vita hiyo haikuanza leo, kwani ilianzia kwenye miradi mingine siku za nyuma hiyo ilituchelewesha kama Watanzania kupiga hatua.

“Rais Dkt. Samia, anatekeleza Ilani ya CCM, kwani mipango ya kukuza uchumi wa viwanda, uwekezaji kupitia sekta binafsi na maboresho ya bandari zetu ikiwemo ya Dar es Salaam, vilishawekwa kwenye Ilani ya CCM ya 2020- 2025, na msingi wa miradi hiyo ilishawekwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Hayati Dkt.John Magufuli,” amesema na kuongeza kuwa

“Tatizo lipo wapi hapo Rais Dkt. Samia, anaendeleza miradi ni kwa sababu mradi huu wa bandari ya Dar es Salaam utaibeba CCM kwenye chaguzi zijazo,ukiona adui anakushangilia unachofanya anza kustuka ila ukiona unafanya jambo halafu adui analalamika, ujue anajua utafanikiwa,” amesema Chongolo.

Wananchi wa Mkoa wa Tanga wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Mazoezi mjini Korogwe ili kuwasikiliza viongozi walioambatana na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

Chongolo amesema Tanzania ikiwa sehemu ya dunia, ipo katika mapambano ya vita vya kiuchumi na kuwataka Watanzania kuwa makini na watu wachache, kwani katikati ya mapambano hayo kuna vibaraka wamepandikizwa ili kuturudisha nyuma kimaendeleo na wanataka kutumia mjadala wa uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam ili kutukwamisha.

“Kama taifa tulitaka kujenga chanzo cha kuzalisha umeme kwenye mto Malagarasi, lakini tukaelezwa hapo tutaharibu mazingira na kuua viumbe adimu ambavyo havipo sehemu nyingine duniani,tukaenda bwawa la Kihansi ili kuzalisha umeme, huko tukaelezwa kuna vyura wapo hapo, na hawapatikani popote duniani,sasa vyura na umeme kipi bora?… bora umeme, na tuliweza kujenga miradi yetu ya umeme ya Mtera, Kihansi na Kidatu, na hakuna uharibifu wowote,”amesema Chongolo.

Chongolo amesema kuwa ingawa nchi imepata Uhuru baada ya kuwaondoa wakoloni, lakini vita iliyopo sasa duniani ni ya kiuchumi ili kushinda vita hiyo kunahitajika akili, busara na mikakati zaidi kupigana na kwamba nchi inatakiwa kuwa imara ili isiyumbishwe wala kutolewa kwenye mipango yake na wapinzani au maadui wasioitakia mema nchi yetu.

“Sasa hivi hatupigani ili kupata Uhuru tena kwa sababu upo,vita ya sasa ni vita ya kiuchumi na hii ni vita ya dunia. sisi Tanzania ni sehemu yake na sisi tunapigana vita hiyo, asubuhi mchana na jioni,wanaTanga na Watanzania wenzangu, vita ya uchumi ni vita ya kutumia akili, busara na ya kimkakati zaidi huwezi kuiona kwa macho wala kuishika kwa mkono, lakini ni vita,”.

“Tena ni vita kubwa, kuliko hata ile vita ya ukombozi wa wakati huo,vita ambayo ukikaa kienyeji umeenda na maji,kwa nini nasema ukikaa kienyeji umeenda na maji, kwa sababu fursa zilizopo tunazipigania wote, kuzipata na kuzitumia ili kujiendeleza, na ni fursa za aina moja na zinapatikana kwenye maeneo yale yale,kwa hiyo kila mmoja anaiangalia fursa kwa jina lake, kwa jicho lake, kwa namna yake na kwa mazingira yanayomzunguka,” amesema Chongolo.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Jokate Mwegelo akiwa na Wakuu wa Wilaya wenzake, na wenyeviti wa CCM wilaya za Mkoa wa Tanga katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Mazoezi mjini Korogwe ili kuwasikiliza viongozi walioambatana na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.

Chongolo amesema serikali ya awamu ya sita ipo kazini na Mkoa wa Tanga unanufaika kwa utekelezaji wa miradi mingi ikiwemo ya barabara ambapo mradi wa barabara kutoka Handeni- Kiberashi, Kibaya (Kiteto)- Chemba- Singida ya kilomita 460 ipo kwenye hatua za utekelezaji kwa kiwango cha lami huku barabara ya Tanga- Pangani- Saadan- Bagamoyo inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema kwa kipindi cha awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia, wamepokea zaidi ya trilioni mbili kama fedha ya miradi ya maendeleo, hivyo kama kauli mbiu ya Tanga inavyosema; “Tanga bega kwa bega na Rais Dkt. Samia”, ndivyo watakavyokwenda vivyo hivyo, kuona wanamuunga mkono kwa kila jambo jema analofanya kwa wanaTanga na Watanzania kwa ujumla.