Na Mwandishi wetu, timesmajira
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale imeendelea kuweka mikakati yake ya kuainisha maeneo ya Ķihistoria yaliyopo wilaya ya Chamwino kwa lengo la kuyatangaza kiutalii ili kwenda sambamba na kasi ya matokeo chanya ya Filamu ya “The Royal Tour”
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale nchini, Dkt. Chistowaja Ntandu alipotembelea Kijiji cha Chamwino kilichopo katika wilaya ya Chamwino kwa ajili ya kubainisha na kukagua maeneo ya Kihistoria pamoja na kukutana na baadhi ya Wazee ili kupata historia ya eneo hilo adhimu
Dkt. Ntandu amesema kuwa, wilaya ya Chamwino ina utajiri mkubwa wa hihistoria unaoenda sambamba na historia ya Muasisi wa Taifa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipopata wazo la kuhamishia Makao makuu ya nchi Dodoma, na utekelezaji wa Sera ya Ujamaa na Kujitegemea kuanzia mwaka 1969 hadi 1974.
“Ikumbukwe hapa ndipo kulipoasisiwa Kijiji cha kwanza cha Ujamaa mwaka 1973 ambapo ndipo palipojengwa nyumba 40 bora za mfano ili wananchi waishi katika mazingira bora, ndipo Ikulu ambayo imesimama kama alama ya Makao Makuu ya nchi na huduma nyingi muhimu za kijamii zilianzia hapa hivyo tunaona kuna fursa ya kuhifadhi na kutangaza eneo hili ili wageni wafike kutembelea kujionea historia hii pindi wanapofika Dodoma” Amesema Dkt. Ntandu.
Aidha, Dkt. Ntandu ameeleza kuwa kuna fursa ya kuanzisha Makumbusho itakayohifadhi historia adhimu ya Chamwino na kuendeleza utajiri huo kama zao la Utalii utakaoendana na kasi ya ongezeko la Watalii nchini kama ilivyoelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii , Dkt Abbas Hassan wakati wa maadhimisho ya Mwaka mmoja wa Matokeo ya Royal Tour.
Akizungumzia hatua inayochukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Wilaya ya Chamwino, Peter Maloda, ameipongeza Wizara hiyo ambayo inaenda kufungua fursa kwa wakazi wa Chamwino kupitia Watalii watakaotembelea maeneo hayo ya kihistoria ambayo ni ya kipekee nchini na wapo tayari kuwakaribisha na kuwapatia historia hiyo.
Katika ziara hiyo, Dkt.Ntandu ametembelea Kisima cha Ipala la Ntembo ambacho kilitumiwa na wananchi kumwagilia bustani za vikundi kabla ya kuanzisha kijiji cha Chamwino, Mti wa Mnyinga uliotumika kwa mikutano, eneo la nyumba kumi za kwanza za kijiji cha Ujamaa.
Maeneo mengine ni pamoja na Nyumba ya Muasisi wa Kijiji Cha Ujamaa cha Chamwino Mzee Lobinaa, Mesi ya chakula iliyotumiwa na watumishi na wageni wa Ikulu, eneo la Kibaraza(Chibalangu) lilotumika kufyatua tofali za ujenzi wa nyumba bora, zahanati ya kwanza na ukumbi wa mikutano.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best