April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chama aendelea ‘kutikisa’ Simba

Na Mwandishi Wetu, Times MajiraOnline

KINARA wa pasi za mwisho za goli ‘Assist’ ndani na klabu ya Simba na Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), Clatous Chama amefanikiwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mashabiki wa mwezi Aprili (Emirate Aluminium Simba Fans Player of the Month).

Katika mechi saba alizocheza Aprili, Chama amehusika katika mabao nane baada ya kufanikiwa kufunga goli tatu huku akiitoa pasi tano za mwisho za goli.

Hiyo ni tuzo ya pili kwa Chama ndani ya mwezi Aprili baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki katika mzunguko wa tano wa mechi za hatua ya Makundi ya michuano ya Ligi Mabingwa Afrika akiwa wa pili baada ya Luis Miquissone kuchukua ya mzunguko wa pili.

Katika wiki hiyo Simba ilifanikiwa kupata ushindi mnono wa goli 4-1 dhidi ya AS Vita katika mchezo uliochezwa Aprili 3 katika uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa na miongoni mwa magoli hayo Chama alihusika katika magoli matatu baada ya kufunga magoli mawili dakika ya 45 na 83 huku akitoa pasi ya mwisho ya goli lililofungwa dakika ya 66 na kiungo Rally Bwalya.

Chama amefanikiwa kutwaa tuzo hiyo baada ya kuwagaragaza kipa Aishi Manula na Beki Shomary Kapombe alioingia nao fainali ambapo katika kura zilizopigwa na mashabiki hao, Chama alipata asilimia 50.48 akifuatiwa na Manula aliyepata asilimia 30.74 huku Kaombe akipata asilimia 18.78 na kura zilizopigwa.

Kiungo huyo anakuwa mchezaji wa tatu kutwaa tuzo hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Emirate Aluminium Profile ambao walinza kuitoa Februari ikichukuliwa Luis Miquissone huku tuzo ya Machi ilienda na beki kisiki, Joash Onyango.

Hivi karibuni nyota huyo wa Simba, aliweka wazi kuwa kwa sasa jambo kubwa kwake ni kuendelea kuitumikia klabu yake kwa ubora wa hali ya juu ili kuweza kuipa mafanikio wanayoyahitaji ikiwemo kuipambania nafasi ya ufungaji bora wa Ligi Mabingwa Afrika.

Hadi sasa katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi hiyo, Chama amefunga goli nne na kukaa kwenye nafasi ya tano katika orodha ya wafungaji bora wa michuano akizidiwa goli tatu na kinara Amir Sayoud wa CR Belouizdad mwenye goli saba huku Saifeldin Malik Bakhit wa Al Merrikh akiwa na goli sita.

Firas Chaouat wa Club Sportif Sfaxien ana goli tano huku Ayoub El Kaabi wa Wydad Casablanca, Chama na Mohammed Ali Ben Romdhane wa Esperence wakiwa na goli nne.

Sasa vita kubwa ipo kwa Sayoud, Kaabi, Chama na Romdhane ambao timu zao zimeshafanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali.

Ikiwa nyota huyo atafanikiwa kupata magoli katika mechi zao zijazo na Simba kusonga mbele zaidi basi atajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania kiatu hicho kwani hadi sasa baadhi ya washindani wake timu zao zimeshindwa kutinga robo fainali.

Lakini mbali na Chama kuwania kiatu hicho nyota wa klabu ya Simba walioingia katika orodha ya wachezaji 150 waliofanikiwa kufunga katika michuano hiyo yupo Luis Miquissone aliyefunga goli tatu huku mshambuliaji Chris Mugalu akifunga goli mbili.