January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chalamila awaasa wajasiriamali wanawake kutoigana

Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wanawake

wajasiriamali kutoigana mawazo ya biashara huku kila mmoja kufanya biashara yake kwa ufanisi.

Chalamila ameyasema hayo, mwishoni mwa wiki, katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Wanawake Wajasiriamali Kutoka Tanzania Bara na Visiwani, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Mama Anna Mkapa na kuhudhuriwa na wanawake Wajasiriamali 100.

RC Chalamila akizungumza na wanawake wajasiriamali kutoka Tanzania Bara na Visiwani, katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam.

Pia amesema kuwa, wanawake hao wanapaswa kuwa na nidhamu ya fedha wanayopata kutoka katika biashara zao, kwani wao ndiyo nguzo katika Jamii.

” Ni vyema mkawa na nidhamu katika kile kipato mnachokipata,hiyo ndiyo silaha yako wewe kama mwanamke,kwani wakina mama wangapi tumeona wamepoteza focus kutokana na waume zao kuwanyanyasa hivyo inabidi kutumia akili sana katika kile unachokipata,”amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za kina mama wote katika kuhakikisha inatoa mikopo kwa asilimia ndogo ili waweze kujikwamua kimaisha.

“Serikali bado inania ya dhati ya kuhakikisha wakina mama wote wanapata mitaji kwa kumuangalia Mama Anna Mkapa bado nyinyi mna nafasi kubwa ya kupata mikopo hiyo kwa kuhakikisha wote mlio katika taasisi hii mnajiunga katika vikundi vya watu wachache na wote mtapatiwa,”amesema Chalamila.

Aidha ameongeza kuwa uwepo wa ndege kubwa ya mizigo ambayo iliingizwa hivi karibuni,itasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara kuweza kusafirisha mizigo yao nje ya nchi kwa wakati.