May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF yatahadharisha utapeli dhidi ya wastaafu

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewatahadharisha Wanachama wake hususan Wastaafu kuwa makini kufuatia aina mpya ya utapeli ambapo wahalifu wa kimtandao wamekuwa wakiwalaghai Wastaafu wanaopokea Pensheni ya kila mwezi.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Julai 2, 2023 na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe ikiwa ni sehemu ya Elimu kwa Wanachama inayotolewa kwenye banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Wahalifu wa kimtandao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kihalifu na sasa wamebuni ujumbe mfupi wa simu (sms) na kumtumia Mstaafu wakimueleza kuwa akaunti yako imefungwa na hivyo kumuelekeza atume taarifa za akaunti yake kwenye namba ambayo usipoiangalia kwa umakimni utaamini kuwa ni namba maalum na siyo ya simu ingawa kimsingi ni namba ya simu, na mstaafu anapotekeleza maelekezo hayo wahalifu wanaingia kwenye akaunti na kuchukua fedha zilizopo.” Alifafanua Bw. Mlowe.

Alisema awali wahalifu hao wa kimtandao walikuwa wanawatapeli wastaafu wakishalipwa kiinua mgongo (Lumpsum Payment) ambapo waliwalaghai kwa kuwaeleza kuwa malipo yao waliyopokea ni pungufu kwa hivyo wao wana uwezo wa kufanya marekebisho ili wapate malipo zaidi wanayostahili.

“Hata hivyo utapeli huu umegonga mwamba baada ya kuwapa elimu ya kutosha wastaafu wetu na ndio maana wamebuni mbinu hii mpya.” Alisema.

Bw. Mlowe amewatahadharisha Wanachama na Wastaafu kutopokea maelekezo yoyote kutoka kwa watu wasiowafahamu wanaotaka kujua kuhusu malipo yanayofanywa na PSSSF.

“Tuna ofisi kila mahali Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, kwa hivyo Mwanachama kama una jambo lolote usilolifahamu kuhusiana na malipo yako wasiliana na ofisi zetu moja kwa moja bila ya kupitia kwa mtu yeyote usiyemfahamu.” Alisisitiza Meneja Huyo wa Uhusiano na Elimu kwa Wananchama.

Aidha mmoja wa wanachama wa PSSSF ambaye anakaribia kustaafu, Mwalimu wa Shule ya Msingi Msasani jijini Dar es Salaam, Bw. Osmund Xavery Hyera, alisema visa vya utapeli kwa wastaafu hata yeye amevisikia na kutoa ushuhuda kuwa mwalimu mwenzake (hakumtaja jina), aliwahi kupigiwa simu wakati akikaribia kupokea mafao ya mkupuo.

“Walimueleza kuwa wao wanauwezo wa kuharakisha Mchakato wa malipo yake kwahiyo wakamtaka atoe taarifa zitakazowezesha zoezi hilo kufanyika.” Alisema Mwalimu Hyera

Alisema ” Hao matapeli walijitambulisha wako TAMISEMI Dodoma, bahati nzuri mtoto wa yule mstaafu akamwambia baba yake asifanye mawasiliano yoyote na kumuachia jukumu hilo alifanye yeye kuwasiliana na  watu hao, alipowataarifu kuwa kuwa amefika TAMISEMI ili kupata ufafanuzi walikata simu.” Alifafanua.

Aidha kuhusu ushiriki wa Mfuko kwenye Maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Tanzania Mahali Salama kwa Biashara na Uwekezaji.” Bw. Mlowe alisema, Wanachama, Wastaafu na Wananchi kwa ujumla wanahimizwa kutembeela banda la PSSSF ili kupata elimu ya hifadhi ya jamii kama vile Taarifa za Michango ya Wanachama, Taarifa kuhusu Mafao mbalimbali yatolewayo na Mfuko, Taarifa za Uwekezaji na fursa mbalimbali zinazopatikana PSSSF na kwa Wastaafu wataweza kujihakiki.

“Sheria inataka Mstaafu kujihakiki mara moja Kila Mwaka, safari hii tuna utaratibu mpya na wakisasa unaomuwezesha Mstaafu kujihakiki.” Alisema

 Zamani Mstaafu alilazimika ku Eva nyaraka wakati anakuja Ofisi za PSSSF kujihakiki, tumeachana na mfumo huo hivi sasa Mstaafu atalazimika kuja na kitambulisho chake cha NIDA au namba ya NIDA na atachukuliwa alama zake za vidole (biometric) na tayari atakuwa amejihakiki na ni mara moja tu kwa Mwaka, Alifafanua Bw. Mlowe.

Sambamba na kuwahudumia wanachama na wastaafu kwenye banda la Mfuko, PSSSF pia imekuja na staili mpya ya kuwatembelea wanachama wake ambao ni watumishi wa Umma wanaoshiriki kwenye maonesho hayo huko huko waliko kwenye mabanda yao kampeni inayokwenda kwa jina la “Banda kwa Banda”.

“Tumeona ni njia nzuri ya kuwahudumia wanachama wetu waliopo hapa Sabasaba, kwa kuwa na wao wanatoa huduma kwa wananchi, sisi tunawafuata huko huko waliko na kuwaelimisha kuhusu matumzi ya huduma za PSSSF Kiganjani na PSSSF ulipo Mtandao.” Alisema Bw. Abdul Njaidi, Afisa Uhusiano Mkuu PSSSF.

Alisema huduma hiyo humfanya mtu anayekabiliwa na majukumu mengi kupata huduma za PSSSF kupitia simu yake ya kiganjani kwa kupakua APP ya PSSSF kwenye simu yake.

“Lakini kampeni hii ya Banda kwa Banda imetuwezesha kugundua kuwa baadhi ya wanachama wetu wanahitaji ufafanuzi tu ili kutatua changamoto ndogo ndogo zinazowakabili kuhusiana na huduma zetu.” alibainisha Bw. Njaidi.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe , akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la PSSSF Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Julai 2, 2023.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe, akizungumza na waandishi wa habari Julai 2, 2023.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, PSSSF, Bw. James Mlowe, akimpa elimu Mwnaachama wa PSSSF, Mwalimu Osmund Xavery Hyera.
Banda kwa Banda; Afisa Uhusiano Mkuu PSSSF, Bw. Abdul Njaidi (wapili kushoto), akiwa na Watumishi wenzake akielezea nia ya kampeni hiyo kwenye banda la Bima. Wapili kulia) ni Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Taifa la Bima (NIC) Karim Meshack 
Banda kwa Banda; Afisa Uhusiano Mkuu PSSSF, Bw. Abdul Njaidi (wapili kushoto), akiwa na Watumishi wenzake akielezea nia ya kampeni hiyo kwenye banda la TBC. 
Banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Banda la NIC
PSSSF Kiganjani
Afisa Mkuu wa Uhusiano PSSSF, Bi. Fatma Elhady (kushoto)  akimuhudumia Mwnaachama wa Mfuko huo Bi. Gisbertha Njako.
Huduma zikiendelea kwenye banda la PSSSF.
Huduma zikiendelea kwenye banda la PSSSF.