May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Chalamila afunguka juu ya wananchi wa Dar es Salaam kufaidika na mkutano wa mifumo ya chakula

Na  David John timesmajira online 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema kuwa kufanyika kwa mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya chakula hapa nchini kunaweza kusababisha kupunguza tatizo la dola ambalo lilikuwepo hapa nchini.

Amesema kuwa hata kwa upande wa vyakula Tanzanaia itaweza kufaidika na hasa kwa Upande wa Dar es Salaam  mkoa ambao ni kitovu cha uchumi wa nchi .

Chalamila ametoa kauli hiyo leo septemba 5 ,2023  kwenye viwanja vya kituo cha mikutano ya Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere  ambapo Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya chakula Afrika  unafanyika .

Amesema kuwa Dar es salaam ndio Kila kitu kwani Kuna wakazi si chini ya milioni tano na ndio kitovu cha masuala mengine yote yanayohusu biashara za kawaida za ndani na nje  huku akisema Dar es Salaam itafaidika sana Kutokana na utalii utakaokuwa unafanywa na wageni mbalimbali wa aliokuja kwenye mkutano huo.

Chalamila ameongeza  kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuja kwenye mkutano huo hadi ukumbi wa Mwalimu Nyerere unaonekana ni mdogo na katika hili inapelekea kupata mawazo ya kuongeza kumbi zingine  na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameshaliona hilo na mapema sana ukumbi huo utaaza kupanuliwa Ili kukidhi mahitaji makubwa ya matumizi.

Amefafanua  kuwa mkutano huo ni miongoni mwa mkutano mkubwa ambao unafanyika katika ukanda huu huku akisema pia kuna mkutano mwingine mkubwa wa shirikisho la  michezo Duniani  ambao utafanyikia hapa nchini .

Amesema kuwa kupitia mkutano huo ambao unatarajia kufanyika hapa nchini tayari vyumba vimeshaaza kubukiwa  na wito wake Kwa wakazi wa Dar es Salaam nikwamba fursa kama hizo haziji mara mbili hivyo wajaribu kutumia fursa hiyo vizuri ili kuweza kupata faida za mkutano huo mkubwa. 

Akizungumzia hali ya usalama Chalamila amesema kuwa mkoa wa Dar es salaam uko salama na hali Iko Shwari na Ulinzi uko Kwa asilimia 100 na hakuna mtu yeyote ambaye atapata itilafu katika kuishi kwake  hapa Dar es salaam kuazia Leo hadi utakapotamatika mkutano huo.

Kuhusu vijana  Amesema kuwa hivi Sasa kilimo sio tena adhabu kama ilivyokuwa huko nyuma  hivi Sasa Rais  Dkt.Samia ameleta kilimo kama biashara ,fursa ,kilimo ni sayansi hivyo vijana waliomaliza vyuo vikuu na ambao hawajamaliza watumie fursa hiyo vizuri na watende Kwa vitendo na waifutilie kweli kweli ili kuweza Kubadilisha maisha yao.