December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kada wa CHADEMA, Andrew Pallaiga akisaini kitabu cha wagombea mara alipowasili katika ofisi za chama hicho kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea Ubunge katika Jimbo la Iringa mjini.

CHADEMA: Tunakwenda kuipoteza CCM kabisa

Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa

KADA wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA), Andrew Pallaiga amechukua na kurudisha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea Ubunge katika Jimbo la Iringa mjini huku akiwahakikisha wafuasi wa chama hicho kulitetea Jimbo na Halmashauri ya Iringa.

Pallaiga amechukua fomu mapema leo katika ofisi za Chadema zilizopo Mjini Iringa nakusema kuwa lengo la kuomba ridhaa hiyo ya kuteuliwa na chama chake ni kuiondoa CCM ambayo ndio adui namba moja kwao.

Amesema kwa sasa chama chao hakina makundi hivyo atakua tayari kushirikiana na mgombea yeyote atakae pitishwa na chama kwa kuwa wote wana malengo ya kuiondoa CCM madarakani.

Ameongeza kuwa mwaka 2015 CCM ilifanikiwa kupata viti 4 vya udiwani lakini msimu huu hawatapata kiti hata kimoja na wala ubunge jambo ambalo litawafanya waendelee kuishikilia halmashauri.

Pallaiga amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuacha kudanganyika na watu wanaopita kwa kuwapa vitu vidogo kama tisheti, vilemba, kanga na fedha badala yake wachague viongozi bora ambao wataenda kuwavusha katika miaka mitano ijayo.

Katibu wa CHADEMA Iringa mjini, Hamid Mfalingundi akifafanua kuhusu utaratibu wa kujaza fomu ambapo wagombea 14 walijitokeza kuchukua fomu.

Katibu wa Chama cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) iringa mjini, Hamid Mfalingundi amesema jumla ya wagombea 14 wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania Ubunge katika Jimbo la Iringa mjini.

Wagombea wanatakiwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na chama ili kuepuke kukatwa majina yao pindi watakapobainika wameenda tofauti na maagizo ya chama.

Amesema wagombea wanatakiwa kufahamu kuwa suala la kuchukua fomu ni lingine na la kuteuliwa pia linasehemu yake kwani wanaingia kwenye vikao vya kuwajadili ili apatikane mmoja atakae peperusha bendera ya chama chadema.