Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewapongeza na kuwashukuru wanachama, viongozi wa chama na jumuiya zake, wabunge, viongozi wa serikali, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wananchi wa Majimbo ya Buhigwe na Muhambwe sambamba na kata zilizofanya uchaguzi kwa kukamilisha kwa salama, amani na mafanikio makubwa chaguzi ndogo zilizokamilika juzi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka kwa vyombo vya habari katika chaguzi hizo wagombea wa chama hicho Jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru alitangazwa mshindi kwa kura 25,274 sawa na asilimia 83.3 ya kura zote na Jimbo la Mihambwe, Dkt. Florence Samizi ameshinda kwa kura 23,441 sawa na asilimia 66 pamoja na wagombea wa CCM katika kata 17 wametangazwa kushinda kwa kishindo.
Amesema, ushindi huo mkubwa wa CCM kwenye Majimbo ya Buhigwe na Muhambwe, pamoja na kata 17 ni zawadi ya wanachama wa CCM kwa Mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan huku wananchi wa Kigoma wakimshukuru Rais Samia kwa kumteua, Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais.
“Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia anatoa shukrani kwa makada wa CCM, viongozi wa Mkoa wa Kigoma, Jumuiya za chama ngazi ya mkoa na taifa waliohakikisha ushindi wa CCM unapatikana,”.
“Chama Cha Mapinduzi kimeendelea kujisahihisha, kujiimarisha na kuwahakikishia Watanzania kuwa Ilani ya Uchaguzi wa CCM 2020/25, itatekelezwa kwa mafaniko makubwa katika maeneo yote kiuchumi, kijamii na kisiasa,” amesema kiongozi huyo.
Pia amesema, CCM itaendelea kusimamia na kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa vyama vyote kufanya siasa safi, zenye tija za kuwaunganisha Watanzania ili taifa lizidi kupiga hatua za kimaendeleo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best