November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM watuma salamu za pole kwa familia ya Hayati Lowassa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeungana na Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipa pole familia ya Hayati Edward Lowasa aliyefariki Dunia leo wakati akipatiwa matibabu hospitali ya Taifa Muhimbili.

Salamu hizo za pole zimetolewa leo na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Songea Mjini Mkoa wa Ruvuma wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi katika mikoa 20 Back to Back ambapo amesema Hayati Lowassa amefariki saa nane mchana kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akitibiwa tatizo la moyo

“Mpendwa, kiongozi wetu, na mwanachama wetu wa Chama Cha Mapinduzi aliyekuwaty Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Lowassa amefariki leo tarehe 10 saa nane mchana katika hospitali ya Moyo pale Muhimbili.

“Chama Cha Mapinduzi kiunaungana na Mwenyekiti wetu na watanzania wote, kuipa pole familia ya Hayati Ngoyai Edward Lowassa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na kumuomba Mungu kwa kudra zake atupe uvumilivu katika wakati huu mgumu wa msiba ambao wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwa kumpoteza mwanachama na familia kumpoteza baba, mjomba na babu” Alisema Makonda na kuongeza kuwa

“Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi tunatoa pole kwa wanachama wapenzi wa Chama chetu,wakereketwa na watanzania wote kwa ujumla kwa kuwa amekuwa kiongozi mwema na kwa nafasi zake zote ametoa mchango kwa Taifa letu” Alisema Makonda

Makonda alisema wakati anaanza ziara yake alifanikiwa kupita katika Jimbo la monduli na kumuongelea mema yake kwani wote walikuwa kwenye Chama hiko

“Wakati tunaanza ziara yetu, Dar es Salaam, tukaenda pwani, tukaenda Tanga, Kilimanjaro, na tulipofika Arusha tulipata nafasi ya kwenda kwenye Jimbo la monduli, kaka yangu Fredy akiwa ndiyo Mbunge, na tulimkumbuka Mzee wetu kwasababu wote tumekuwa kwenye Chama hiki na katika Utumishi wa serikali tukiwafahamu viongozi wetu

Hatukujua ya kwamba kabla ya kumaliza ziara yetu tutapata taarifa nzito na ngumu kama hizi lakini yote ni mapenzi ya mungu”

Pia Makonda alisema Hayati Edward Lowassa atakumbukwa kwa mambo mengi lakini pia kwa umahiri wake wa kujenga hoja katika nyakati tofauti na kufanya kazi katika Taifa letu lakini

“Kwa mapenzi ya mwenezi Mungu hatuna budi kukubaliana”

Kadhalika kutokana na Rais Dkt. Samia kutangaza maombolezo na kushusha bendera kwa siku 5, Makonda amesema wao kama Chama wanajipanga kusubiri utaratibu ili wanachama wote waweze kujulishana na namba watakavyoshiriki katika kumuhifadhi katika nyumba yake ya milele.

“Mhe. Rais ametangaza maombolezo na kushusha bendera kwa siku 5, kupitia tangazo hilo la kiongozi wetu na Mwenyekiti wetu wa Chama, na sisi kama Chama tutajipanga kusubiri utaratibu ili wanachama wote tuweze kujulishana hatua na namna tutakavyoshiriki katika kumuhifadhi katika nyumba yake ya milele

Mengi tutayapa na mengi tutayasema kadri ya ratiba na viongozi wetu wakuu wanavyotuelekeze” Alisema Makonda

Lowassa alihidumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania chini ya Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa miaka mitatu toka 2005-2008.

Pia Hayati Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 na amefariki akiwa na umri wa miaka 70 ambapo anaacha alama kama Moja ya miamba ya Siasa za Tanzania