May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CBE kufundisha Online

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimesema kuanzia mwakani kitaanza kufundisha baadhi ya kozi zake kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha watu wengi kusoma masomo hayo ya biashara.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga wakati wa kongamano kuelekea mahafali ya 58 ya chuo hicho yanayotarajiwa kufanyika kesho Ijumaa katika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam.

Alisema CBE imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha wanatoa wahitimu bora zaidi na wameshasaini mkataba na Wakala wa Vipimo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Elimu Mtandao (e Government) kwaajili ya kuendesha program za uanagenzi na atamizi.

“Sasa hivi tumeona elimu tunayotoa tuiboreshe iwe bora zaidi kwa hiyo tunatarajia baada ya hiyo mikataba kusainiwa kuanzia mwakani tutaanza kutoa mafunzo ya metrolojia kwa vitendo zaidi ambayo yanakuwa ya uanagenzi kwa wanafunzi wetu kusoma na kwenda kufanyakazi kwa vitendo,” alisema

Alisema pamoja na kuboresha uhusiano na vyuo na taasisi za ndani ya nchi, CBE imeendelea kuimarisa uhusiano na vyuo vya nje ya nchi na kwa sasa wafanyakazi nane wa chuo hicho wanasoma Shahada za Uzamivu (PhD) nchini China kwenye uchumi na uhasibu.

Alisema pia chuo hicho kina uhusiano mzuri na Chuo cha Eastern University cha Finland ambako wamekuwa wakizalisha wataalamu wa fani ya Business Informatics na walimu watano wameshahitimu ngazi ya PhD na wengine wanaendelea na masomo yao.

Alisema katika kuboresha tafiti za chuo hicho na taaluma, chuo kimeendelea kufanya makongamano kujadili masuala mbalimbali kila mwaka na mwaka na mwaka huu kongamano hilo litafanyika mkoani Dodoma.

Alisema mgeni rasmi kwenye kongamano hilo la biashara anatarajiwa kuwa Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete na mada itakuwa biashara na mazingira ya uwekezaji.

Alisema CBE imekuwa ikiboresha mitaala na katika kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa kuingiza sokoni program 10 kuanzia ngazi ya Stashahada mpaka Shahada ya kwanza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Stella Kahwa alisema kwa sasa nchi inahitaji vijana wabunifu watakaoweza kuziweka nadharia za darasani katika vitendo.

“Nimetembelea maonyesho yenu nimeona ubunifu mbalimbali wa wanafunzi na hata wajasiriamali ambao wamepitia program atamizi wameweza kufungasha bidhaa zao kitaalamu sana mpaka nimeshangaa na zimefikia viwango vya kimataifa,” alisema

Alikipongeza chuo hicho kwa kuanzisha progamu atamizi na ya uanagenzi ambayo imewezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo na kuvunja mipaka ya nadharia kwa kufanya miradi ya utafiti kwa vitendo.

Alikipongeza chuo hicho kwa kuendelea kuimarisha, kuboresha miundombinu ya chuo hicho na mageuzi makubwa waliyofanya kutoka idara moja na sasa kuwa na zaidi ya kozi 30 za ngazi mbalimbali kuanzia Cheti hadi Shahada za Uzamili.

Alisema mwanzoni chuo hicho kilikuwa na walimu wachache wenye Shahada za Uzamivu na Uzamili lakini sasa wameongezeka mara dufu na wamesaidia kutoa wahitimu bora ambao wanaweza kuajiriwa hata nje ya nchi.

“Nilikuwa mwanafunzi wa chuo hiki kozi ya metrolojia wakati huo chuo hakikuwa hivi nimeshangaa sana kuona mageuzi makubwa nakumbuka nilikuwa msichana pekee kwenye darasa la wanafunzi 25 wa metrolojia,” alisema Stela ambaye alihitimu katika mahafali ya 23 ya chuo hicho miaka 35 iliyopita.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Latifa Khamis alisema mafanikio ya chuo hicho yanamfanya ajiskie fahari kuwa mhitimu wa chuo hicho.

Alisema amefanikiwa kuwa mwanachama wa mtandao wa wataalamu wa masoko nchini kutokana na msingi mzuri alioupata chuoni hapo hali ambayo imemfanya kupenda fani.

“ Kwa kasi hii ya mageuzi ndani ya CBE basi yajayo yanafurahisha sisi Tantrade tumeongea na mkuu wa chuo kuna mambo mengi sana tutashirikiana na chuo kuwatangaza maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi,” alisema