Na Joyce Kasiki, Geita
NISHATI ya Briquettes imeelezwa kuwa miongoni mwa fursa zinazoweza kusaidia Watanzania kupunguza gharama za nishati ya kupikia huku wakichangia utunzaji wa mazingira.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kisome Enterprises, Elias Kisome, baada ya kutembelea banda la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Kisome amesema elimu aliyopata katika banda hilo imemsaidia kutambua fursa zilizopo katika matumizi ya nishati hiyo, akibainisha kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa kuwaelimisha wananchi kuhusu faida za nishati safi ya kupikia.
Amesema kwa mujibu wa wataalamu wa STAMICO, tani moja ya makaa ya mawe inauzwa kati ya Shilingi laki nane na milioni moja na inaweza kutumika kwa muda mrefu, jambo ambalo linaweza kumsaidia mtumiaji kupunguza matumizi ya mara kwa mara ya mkaa wa miti.
“Nimejifunza kitu kikubwa hapa,hii ni fursa kubwa kwa Watanzania, hususan wa vijijini, kuelimishwa kuhusu nishati hii mbadala,” amesema Kisome.
Amesema matumizi ya nishati hiyo yanaweza pia kusaidia kupunguza utegemezi wa mkaa wa miti, ambao uzalishaji wake unahusishwa na ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande mwingine, Kisome amewataka wananchi kujiandaa mapema kukabiliana na mvua zinazotarajiwa, ikiwamo kuweka akiba ya nishati ya kupikia ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua.
Aidha, amewashauri wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi kuchukua tahadhari mapema, ikiwamo kuhama katika maeneo hayo endapo mamlaka zitatoa maelekezo, ili kupunguza uwezekano wa madhara.

More Stories
Wananchi Arusha wapokea kwa hamasa Mkutano wa IPU
Diamond Platnumz asifu miaka 10 ya Tulia Trust
Paradise Mission yawabeba kielimu vijana 100 wa mazingira magumu