September 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Arusha wapokea kwa hamasa Mkutano wa IPU

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

WANANCHI wa Jiji la Arusha wamepokea kwa hamasa kufanyika kwa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), wakieleza kuwa ujio wa viongozi na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ni fursa muhimu kwa jiji hilo na Tanzania kwa ujumla.

Mkutano huo unatarajia kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha, AICC,ambao utakutanisha zaidi ya wageni 200 kutoka sehemu mbalimbali duniani, hali ambayo imeongeza shughuli katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Baadhi ya wananchi wamesema ujio wa wageni hao unatoa fursa kwa wafanyabiashara, watoa huduma za usafiri, hoteli, migahawa na sekta nyingine zinazohusiana na shughuli za wageni.

Wakazi hao pia wameeleza matumaini yao kwamba mkutano huo utasaidia kulitangaza zaidi Jiji la Arusha na Tanzania kimataifa, kutokana na nafasi ya wageni hao kujionea mazingira, utamaduni na shughuli mbalimbali zinazofanyika nchini.

Kwa wafanyabiashara, ujio wa wajumbe wa IPU ni wakati wa kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma na kuhakikisha wageni wanapata huduma zinazokidhi viwango vinavyotarajiwa.

Aidha, wananchi wameeleza kuwa ni jambo la kujivunia kwa Arusha kupewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa kimataifa unaowakutanisha wawakilishi wa mabunge kutoka nchi mbalimbali.

Wakati mkutano ukiendelea, matarajio ya wananchi ni kuona fursa zitakazotokana na tukio hilo zikiwanufaisha zaidi wakazi wa Arusha na kuchangia katika kukuza shughuli za kiuchumi na utalii katika jiji hilo.

Aneth John Mkazi wa Arusha Mjini amesema kuwa ujio wa mkutano huo unawapa fursa wao kama wafanyabiashara kuuza zaidi bidhaa zao hususani vitu vya Kitamaduni.

“Tunashukuru Serikali kwa ujio wa mkutano huu kufanyika jijini Arusha,tunaona ni namna gani tunaenda kuongeza uchumi wa moja kwa moja kwa sisi wananchi tunaoishi mkoa huu,”amesema.