
Na Israel Mwaisaka, Nkasi
TAASISI ya Mvimwa ya kanisa katoliki jimbo la Sumbawanga imekubali ombi la diwani wa kata ya Kate la kuwapelekea maji Wananchi katika vijiji vya Ntemba na China kutoka katika chanzo cha maji Cha mto Katola.
Akizungumza na Majira Diwani wa kata hiyo ya Kate Dismas Msangawale alisema kuwa aliiomba taasisi hiyo ya Mvimwa iweze kuwasaidia Wananchi wa kata hiyo kupunguza tatizo la maji lililodumu kwa muda mrefu Sasa.
Alisema kuwa kufuatia maombi hayo taasisi hiyo Sasa imekubali kupeleka maji katika vijiji viwili vya Ntemba na China na mradi huo kuanza kutekelezwa jumatatu Septemba 28,2026.
Diwani huyo alifafanua kuwa mradi huo utagharimu Tshs,Mil.158 na kuwa mradi huo utakamilika Januari 2026 na kuondoa kabisa tatizo la maji katika vijiji hivyo.
Msangawale alidai kuwa kwa mujibu wa taasisi hiyo ya Mvimwa wao wanao wataalamu wa kutosha watakaofanikisha utekezaji wa mradi huo na kuwa watakachokihitaji kutoka kwa Wananchi ni nguvu Yao tu ya kuchimba mifereji ya kupitisha mabomba ya maji.
Alidai kuwa Wananchi kwa upande wao wameihakikishia taasisi ya Mvimwa Kutoa ushirikiano wa kutosha wa namna yoyote wakati wa utekelezaji wa mradi huo kwani umekuja kuwasaidia kuondokana na changamoto ya maji ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Alisema kuwa hadi sasa wamefanikiwa kuwafikia Wananchi wa vijiji hivyo na kuzungumza nao kupitia mikutano ya hadhara na kukubaliana namna ya ushiriki wao wakati wa utekelezaji wake ili kuhakikisha usiwepo mkwamo wowote ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Kata ya Kate ni moja ya kata zenye changamoto kubwa ya maji licha ya kuwepo kwa vyanzo vingi vya maji .

More Stories
Briquettes yaibua fursa kupunguza gharama nishati kupikia
Wananchi Arusha wapokea kwa hamasa Mkutano wa IPU
Diamond Platnumz asifu miaka 10 ya Tulia Trust