Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa wajasiriamali wengi nchini hawana uelewa wa kutosha kuhusu miliki bunifu hali inavyoweza kuchochea migogoro ya kibiashara pindi anapotokea mtu kughushi alama za biashara zao.
Katika kutatua changamoto hiyo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA),imeanza kutoa mafunzo ya miliki bunifu kwa wafanyabiashara mkoani Mwanza ambayo yatatolewa kwa Wilaya zote mkoani hapa kuanzia Novemba 13 hadi Novemba 16 mwaka huu.
Akizungumza katika mafunzo hayo kwa Wilaya ya Nyamagana ambayo yamefanyika Novemba 13,mwaka huu jijini Mwanza ambapo jumla ya wafanyabiashara 50 wa Wilaya hiyo wamepata mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa sehemu ya Hataza Kurugenzi ya Miliki Bunifu kutoka BRELA Neema Kitala ameeleza kuwa wajasiriamali wengi hawana uelewa juu ya suala hilo.
Hivyo BRELA imeamua kuwafuata wajasiriamali hao ili kuwapa elimu juu ya suala hilo lengo ni kuwaelimisha namna bora ya kutumia bunifu zao na kupeleka bidhaa zao sokoni.
“Tumekuja kutoa elimu ya miliki bunifu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati na tutatembelea Wilaya zote za Mkoa wa Mwanza kwa siku 5 za wiki hii kuanzia Novemba 13 hadi Novemba 16 mwaka huu,tunategemea kupata washiriki wengi katika mafunzo haya ambao watakuwa kama mabalozi kwa wenzao kuweza kuja kurasimisha miliki bunifu zao na kupeleka bidhaa zao sokoni,” amesema Kitala.
Sanjari na hayo ameto wito kwa wafanyabiashara kurasimisha biashara, alama zao za biashara pamoja na huduma ili kuweza kutambulisha bidhaa zao sokoni na kuepesha migogoro inayoweza kutokea baadae.
“Unapata usajili ili ulindwe kisheria kwani mtu yoyote anaweza kuzitumia alama zako na ukipeleka kesi mahakamani hautolindwa kisheria,wito wangu kwa wafanyabiashara warasimishe biashara zao pamoja na alama zao za biashara na huduma ili kuweza kutambulisha bidhaa zao sokoni,”amesema Kitala.
Kwa upande wake Ofisa Sheria Kurugenzi ya Miliki Bunifu kutoka BRELA Calvin Rwambongo ameeleza kuwa sheria ya usajili ya alama ya biashara imeletwa mahususi kwa ajili ya kuwalinda wazalishaji wa bidhaa na watoaji wa huduma ambao wanabuni nembo au michoro mbalimbali katika kutofautisha bidhaa zao na za wengine sokoni.
Calvin amesema kuwa wanajua biashara ni ushindani inatokea mtu anatumia alama ya mwingine ili waweze kutatua migogoro hiyo ndio maana BRELA wanaingia kati kwa ajili ya usajili wa alama za biashara na ulinzi wake unapatikana tu endapo alama imesajiliwa.
Amefafanua kuwa sheria ya usajili wa alama za biashara inaweka wazi kwamba alama ambayo imeisha sajiliwa hamna mtu mwingine atakaye ruhusiwa au kuzitumia alama hiyo pasipo kupata idhini ya mwenye alama.
“Sasa ukishindwa kusajili maana yoyote ataitumia atakuchukulia wateja na ataingiza bidhaa sokoni migogoro itaingia,sisi kama BRELA kupitia sheria hiyo tunatoa vyeti vya usajili wa alama za biashara kwa mtu,mjasiriamali au mfanyabiashara kwa maana hiyo tunakuwa tumempa haki ya kipekee ya alama’ hiyo kuzalisha bidhaa,” amesema Calvin.
Amesema kuwa ikitokea mtu ametumia alama ya mwingine ataenda mahakamani au Tume ya Ushindani ili kupeleka malalamiko yake na endapo imibainika ameiga alama yake au nembo yoyote anayotumia kwenye bidhaa na imesajiliwa basi bidhaa zile zitataifishwa na kuteketezwa pia anaweza kuamuriwa kumlipa fidia mmiliki halali wa nembo husika.
Amewasisitiza na kuwaasa wafanyabiashara kupeleka alama zao za biashara zisajiliwe na ubunifu mwingine zinazohusiana na bidhaa au michakato waipekeke ili wapate vyeti ya usajili au hataza ili kuwa na uthibutisho kuwa wao ndio wamiliki halali na kuepuka migogoro ambayo inaweza kujitokeza baadae.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mkurugezi wa Primina Investment Company LTD Wilhelmina Kubingwa ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wataweka utaratibu mzuri kwa kile wanachotarajia kuzalisha.
Hivyo ameiomba BRELA kuwawezesha mawakala wao wanaofanya kazi kwa niaba yao mikoani kuwapa uelewa juu ya walichojifunza kuhusu miliki bunifu.
“Mawakala wengi upande wa miliki ubunifu hawana uelewa tunategemea nchi nzima BRELA watatembea kutoa elimu ili iweze kutusaidia sisi wafanyabiashara naamini wapo wafanyabiashara wengi wanatamani kuingiza bidhaa zao kwa kushirikiana na viwanda vinavyozalisha,”amesema.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu